WANANCHI wamehakikishiwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utafanyika kama ulivyopangwa.
Ukweli huo unazingatia uwezo wa sasa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wa kuandikisha Watanzania wote wenye sifa ndani ya siku 60, kabla ya Julai, uwezo ambao utakamilisha kazi hiyo ndani ya siku 30.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, Jenista Mhagama ambaye alisema kabla ya Julai, NEC itakuwa na uwezo wa kuandikisha Watanzania 800,000 kwa siku.
Akijibu hoja za wabunge mbalimbali na hasa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), Jenista alisema; “hivi sasa zipo BVR Kit (mashine za kutumia teknolojia ya uchukuaji wa alama za vidole) 4,850. “Tukisema tuzisambaze zote kwenye mikoa mbalimbali kuandikisha wapigakura, tutatumia takribani siku 60 kumaliza kazi, sasa si miezi miwili hiyo, kwa nini tusifanye uchaguzi?”
Akifafanua zaidi kwa takwimu, Jenista alisema siku chache zijazo, Serikali inatarajia kupokea mashine BVR nyingine 3,150 ambazo zitafanya NEC iwe na jumla ya mashine hizo 8,000.
Alisema uwezo wa mashine moja ya BVR wa chini ni kuandikisha watu 100 na uwezo wa juu ni watu 150, mashine hizo 8,000 kwa kadirio la chini, zitakuwa na uwezo wa kuandikisha watu 800,000 kwa siku moja.
“Sasa tuseme tunatumia BVR 7,000, tuweke uwezekano wa mashine 1,000 kuharibika, zikitumika zote 7,000 kuandikisha wapiga kura na tuseme kwa siku BVR moja itaandikisha watu 100, kwa siku 25, tutaandikisha watu milioni 17,” alisisitiza Jenista.
Alisema kuwa iwapo mashine hizo zikitumika kuandikisha watu 100 kwa siku, ni wazi kuwa ndani ya siku 30 kazi ya uandikishaji ya makadirio ya watu milioni 24 itakamilika na daftari la kudumu la mpigakura litakuwa limekamilika.
Kazi inayoendelea
Alitoa mfano wa mikoa ambayo imeshaanza kazi ya uandikishaji kuwa ni pamoja na Njombe, ambao umeshakamilisha kazi hiyo na sasa kazi hiyo iko kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Iringa na Ruvuma.
Aidha, mikoa minane ya Dodoma, Kagera, Katavi, Rukwa, Tabora, Singida, Kigoma, Mbeya itaanza kazi ya uandikishaji kesho na kwamba kazi hiyo itaendelea kwa mikoa mingine hadi ikamilike.
“Uchaguzi upo palepale na wananchi ninawaomba mjiandae na mjiandikishe kwenye daftari la kupiga kura, muda ukifika mchague viongozi bora na Serikali imejipanga kusimamia jambo hilo lifanyike kwa amani na utulivu,” alisema Jenista.
Ushirikishwaji
Kuhusu madai kuwa wadau hawakushirikishwa, Jenista alisema NEC imefanya vikao zaidi ya vitatu kabla ya kuanza kwa uandikishaji na wakati wa uandikishaji na kukaribisha viongozi wakuu wa vyama, asasi za kijamii na mashirika ya dini.
Alisema kama viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa wanabisha, atakuwa tayari kutoa taarifa ya mahudhurio ya viongozi hao hadharani, itakayoonesha pamoja na mambo mengine posho walizolipwa.
Kuhusu hoja ya Serikali kukataa ushauri wa mshauri mwelekezi, Jenista alisema maelekezo ya mshauri mwelekezi yalikataliwa kwa kuwa aliitaka NEC kuboresha madaftari yote mawili kwa pamoja, jambo ambalo ni gharama.
“Serikali na NEC tulikataa kufuata ushauri huo, kwa sababu si kila ushauri tutaufuata, tunaangalia na ushauri wenye tija na kama tungekubaliana na mshauri huyo, maboresho ya daftari hilo yangetumia Sh bilioni 321 zaidi,” alisema Jenista.
Alisema serikali iliona si busara kutumia kiasi hicho kikubwa cha fedha hasa ukizingatia hali halisi ya mapato ya nchi hivi sasa sio mazuri.
Kura ya Maoni haijavunja sheria yoyote-Dk Migiro
Kura ya Maoni
Naye waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro, amesema katika suala la Kura ya Maoni, hakuna sheria iliyovunjwa kutokana na Serikali kuendelea kusisitiza kuwa Kura hiyo itakuwepo.
Amesema hayo alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema), aliyesema kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imevunjwa, kwa sababu iliweka muda wa kufanyika kwa kura hiyo.
Akifafanua hoja hiyo, Dk Migiro alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ilikuwa ikisimamia kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa, ambapo baada ya Bunge Maalumu la Katiba kushindwa kuipata katika muda wa awali, liliongezewa muda kwa kufuata sheria hiyo.
Kwa mujibu wa Dk Migiro, Kura ya Maoni inatawaliwa na Sheria ya Kura ya Maoni ambayo ni tofauti na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika Sheria hiyo ya Kura ya Maoni, Dk Migiro alisema kuliwekwa masharti kuwa kabla ya kufanyika, kutakuwa na muda wa kutoa elimu kwa wananchi.
Alifafanua kuwa asasi za kiraia zinazotaka kufanya kazi hiyo, zimeshapeleka maombi. Dk Migiro alisema kwa kuwa uboreshaji wa daftari hilo ni sehemu ya masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni, iliachiwa chombo kinachohusika ambacho ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutoa taarifa.
Kwa mujibu wa Dk Migiro, kwa kuwa Nec ilitoa taarifa kuwa haiwezi kukamilisha Daftari hilo kwa muda uliokuwa umepangwa, Serikali isingeweza kulazimisha kura hiyo kwa kuwa hata msimamizi wa kura yenyewe ni Tume hiyo ndio maana inasubiriwa ieleze lini itakuwa tayari.
Post a Comment