Loading...

HABARI NZITO YA LEO: CHAMA CHA WANANCHI (CUF) CHA UONA UGAIDI ZANZIBAR

Vurugu Zanzibar
JOTO la kisiasa visiwani Zanzibar halijapoa na sasa Chama cha Wananchi (CUF) kinakuja na tamko zito hivi karibuni, anaandika Michael Sarungi.
Chama hicho kinaeleza kuwa, maisha ya dhiki, wasiwasi, mashaka na unyama uliokithiri katika baadhi ya nchi zinazotawaliwa na ugaidi duniani yanatokana na watawala kudhani kwamba wao ni sehemu ya familia ya Mungu.
Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara ameueleza mtandao huu kuwa, nchi za Nigeria, Somalia na nyingine Afrika zimetawaliwa na vitendo vya kigaidi kutokana na serikali zao kudhulumu wananchi wao jambo ambalo limewapa mwanya magaidi kupata wafuasi.
“Hata haya matukio mengi ya kigaidi tunayoyashuhudia katika nchi kama Nigeria, Somalia na kwingine ni matokeo ya watawala kudharau matakwa ya wananchi kwa kudhani kuwa, wao ndio wenye maamuzi dhidi ya maisha yao ya kila siku,” anasema na kuongeza, matakwa ya Wazanzibari yamepuuzwa.
Amesema, demokrasia ni utawala wa watu, uliowekwa na watu na kwa ajili ya watu tofauti na hapo ni udikteta uchwara.
Amesema pamoja na Tanzania kuridhia mikataba mingi ya Umoja wa mataifa juu ya amani, lakini imekuwa bingwa wa kuikanyaga.
“Demokrasia maana yake ni utawala wa watu, uliowekwa na watu kwa ajili ya watu, kinyume cha hapo ni udikteta unaolenga kulinda maslahi ya watu wachache,” amesema Sakaya.
Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo na amani kwa kipindi kirefu na kuwa, tuendako huenda mambo yakawa tofauti.
“Hapa nchini kuna watu wanadhani wana ukoo na Mungu kwa kudhani kuwa Tanzania haiwezi kutawalika bila yao, huko ni kujidanganya, ipo siku ukweli utajitenga na uongo,” amesema Sakaya.
Amesema, wanatarajia kukutana kama chama na kutoa msimamo mzito juu ya ukandamizaji wa haki za wananchi uliofanyika visiwani Zanzibar ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanaCUF kubambikiwa kesi, kuswekwa rumande bila sababu.
“Tunatarajia kukutana kama chama na kutoa maamuzi mazito juu ya mstakabali wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa ujumla,” amesema Sakaya.
Amesema viongozi wengi wa kisiasa kwa sasa wanaotanguliza maslahi binafsi badala ya wananchi “na ndio maana dunia nzima imeshuhudia sauti ya wengi ikikataliwa visiwani Zanzibar.”

CHANZO: MWANAHALISIONLINE

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright NEWZ | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top