Loading...

Waziri aliyetumia 'Mawe Matatu' kushinda ubunge


Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, amebainisha kwamba alipoingia kwenye kampeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010, alilazimika kuapa mahakamani dakika za mwisho kabla ya siku ya kupiga kura ili jina lake la utani alilopewa na wananchi ‘mawe matatu,’ liingie kwenye karatasi za kupigia kura.
 
Kitwanga tangu mwaka 1988 mpaka 2010, alifanya kazi Benki Kuu ya Tanzania (BoT),  akiwa na nyadhifa mbalimbali kama Mtaalam wa Teknolojia ya Habari (IT), Ofisa Utawala na Naibu Mkurugenzi wa Benki anayeshughulikia uundaji wa mifumo ya utawala.
 
Aliingia Bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010, baada ya kutumia jina hilo la utani na kupata kura 41,935 sawa na asilimia 83.24, Novemba 2010  aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekonolojia, wakati Machi 2012 akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Januari 2014 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini mpaka Novemba 2015.
 
“Ninaitwa Mawe Matatu kwa sababu ya sehemu ninayotoka, ndipo yalipo mawe matatu yaliyoko kwenye noti ya Sh. 500 ya zamani.
“Kitu kilichotokea nilipokwenda kugombea, watu wakawa wanauliza. Hivi huyo ni nani? Wakawa wanaambiwa ni yule fulani anatokea pale kwenye mawe matatu. basi ikawa yule Mawe Matatu, yule Mawe Matatu. mwishowe jina langu wakalisahau.
 
“Ilibidi wakati wa upigaji kura niende mahakamani nikaape, kwa sababu watu hawajui Kitwanga wanajua Mawe Matatu. Ikabidi jina likawa Charles Kitwanga Mawe Matatu,” alisema.
 
Alisema mawe hayo matatu yapo nyumbani kwao, “yaani yalipo hayo mawe matatu, hapo ni nyumbani kwangu, kwa hiyo nilipata identification (utambulisho) wa bure kabisa." alisema na kuongeza:
 
“Watu wanasema haya mawe yapo kama yanayumba, lakini mimi hata siku moja sijawahi kuona yakiyumba. Na uhalisia, yale mawe yapo manne, lakini ukiwa barabarani, unaona yapo matatu, lile la nne halionekani wananchi wengi huwa hawalioni,” alisema.
 
Kitwanga ambaye ni Mbunge wa Misungwi, alisema tangu kuingia kwake madarakani mpaka sasa amepandisha mapato ya halmashauri yake kutoka wastani wa Sh. milioni 250 mpaka Sh. bilioni 1.3.
 
“Mwaka 2010, wakati naingia, tulikuwa tunakusanya Sh. milioni 250 kwa mwaka, baada ya kuziba mianya tukapanda mpaka Sh. milioni 800, tukaja 900 na kitu na mwaka 2015, tulikusanya Sh. bilioni 1.3,” alisema Kitwanga.
 
Alisema mafanikio hayo yalipatikana baada ya kuondoa viongozi wabadhirifu kwenye halmashauri hiyo ambao baadhi yao walikuwa wakitumia kampuni zao kutekeleza miradi chini ya kiwango.
 
“Sasa huwezi kuwa kiongozi kampuni yako ikifanya vibaya halafu nikae kimya, lakini wananchi walinielewa ndiyo maana nilipata ushindi mkubwa mno mwaka jana,” alisema Kitwanga.
 
Katika mchakato wa kutafuta mgombea ndani ya CCM, mwaka 2015, Kitwanga alipata kura 26,171 sawa na asilimia 69.9 dhidi ya mpinzani wake wa karibu ndani ya chama Jacob Shibiliti aliyepata kura 7,009 sawa na asilimia 18. 
 
Katika uchaguzi mkuu, Kitwanga alipata kura 72,072 dhidi ya mpinzani wake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Leonidas Kandela, aliyepata kura 18,050.
 
SOURCE: NIPASHE

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright NEWZ | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top