Baadhi ya wadau wanapendekeza kodi hiyo, inayoitwa excess charge, ipunguzwe kumpa unafuu mfanyakazi, huku wengine wakishauri kuweka nguvu kwenye uchumi wa viwanda na kilimo na baadhi wakishauri juhudi zifanyike kudhibiti mfumuko wa bei ili mshahara utosheleze mahitaji ya mfanyakazi.
Baadhi ya wadau wanapendekeza kodi hiyo, inayoitwa excess charge, ipunguzwe kumpa unafuu mfanyakazi, huku wengine wakishauri kuweka nguvu kwenye uchumi wa viwanda na kilimo na baadhi wakishauri juhudi zifanyike kudhibiti mfumuko wa bei, ili mshahara utosheleze mahitaji ya mfanyakazi.
Juzi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Rais alitangaza kupunguza kodi ya PAYE kutoka asilimia 11 hadi tisa, lakini kwa mujibu wa wahasibu uamuzi huo ni punguzo la Sh1,100 kwa wafanyakazi wa mshahara wa kima cha chini na Sh3,800 kwa mshahara unaoanzia Sh360,000 na kwenda juu.
Akifafanua kuhusu PAYE, mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Richard Kayombo alisema kiwango cha mapato kisichozidi Sh170,000 hakina kodi, lakini mapato ya kati ya Sh170,000 hadi 360,000 yalikuwa yanakatwa asilimia 11 na hivyo sasa yatakatwa asilimia tisa.
Alisema mapato yanayoanzia Sh360,000 hadi 540,000 hukatwa PAYE pamoja na asilimia 20 ya excess charges, wakati mshahara unaozidi Sh540,000 hukatwa PAYE pamoja na asilimia 25 ya makato ya excess charges.
Suala hilo pia lilizungumzwa na mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, Godlisen Malisa katika waraka alioutuma kwenye mtandao kuchambua punguzo hilo la Rais Magufuli.
Malisa alionyesha kushangazwa na kitendo cha baadhi ya watu kusifu punguzo hilo, wakiwamo wabunge wa upinzani.
“Kama Rais angepunguza excess charges, angalau zikafika 10% kutoka 30% ziliko sasa, ingekua na maana kubwa sana kuliko kupunguza PAYE,” anasema Malisa katika waraka huo.
“Kwa kifupi ni kuwa punguzo hilo litawanufaisha zaidi wenye mishahara chini ya 720,000/= lakini kwa wanaolipwa zaidi ya hapo hakuna benefit (manufaa) yoyote. Hata hao wanaolipwa chini 720,000/= bado watanufaika kidogo sana.”
Alidai kwamba kama kuna mbunge yeyote anayeshangilia punguzo ni wazi kuwa hajui hesabu, hivyo anatakiwa kukumbushwa ili aelewe kuwa kupunguza PAYE wakati makato yanayozingatia viwango vya mishahara yako palepale, ni kiini macho.
“Yaani Rais JPM alichofanya ni kutulazimisha tukatae ongezeko la mshahara,” anasema.
Alisema ni kweli wapinzani waliomba PAYE ipunguzwe tangu mwaka 2011 kwamba isomeke kwa tarakimu moja na ndivyo alivyoahidi JPM, lakini pia walishauri kuwa gharama za makato hayo ya zaidi yalingane.
“Nimeamua kusema hivi maana naona wabunge wengi wa (vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi) Ukawa wanacheza ngoma ya Magufuli. Wanaanza kujitapa (kwamba) upinzani tulishauri jambo hili tangu mwaka 2011,” anasema.
“Wengine wanapiga picha hadi hotuba ya kambi ya upinzani iliyozungumzia jambo hilo. Waambieni wakae kimya na wasiendelee kuongea vitu wasivyovijua.”
Mtaalamu wa masuala ya kodi, Dk Mariam Nchimbi alisema kiwango cha mshahara kingepandishwa ni wazi kingesaidia wengi kujipanga vyema, ikiwa ni pamoja na kuendelea kulipa kodi zinazostahili.
“Ni wazi kwamba kwa hatua hiyo ya Rais imewasaidia kwa kiasi fulani wale wanaolipwa mishahara ya kiwango cha kati, lakini wale wa kiwango cha juu pia walipaswa kupunguziwa japo kwa asilimia 28 badala ya 35 inayokatwa sasa,” alisema.
Lakini wachambuzi wengine waligeukia suala la kukuza uchumi wakisema ndilo litakalosaidia mfanyakazi kunufaika na mshahara wake.
Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema mshahara wenye nafuu kwa maisha ya wafanyakazi wengi utapatikana kutokana na uwepo wa viwanda vya kutosha pamoja na kilimo kuimarishwa.
“Kuna mambo mengi ya kuangalia ili mfanyakazi awe na mshahara ambao unampa unafuu wa maisha,” alisema Profesa Moshi.
“Pato la Taifa linahusika kwa kiasi kikubwa, hivyo kama litajengewa mazingira ya kukua, itakuwa vyema. Inatakiwa viwanda vichangie pato hilo kwa asilimia 25 na si asilimia nane kama ilivyo sasa.”
Alisema anaamini baadhi ya viwanda hivyo vitakuwa vya kusindika mazao, kutakuwa na kilimo cha biashara ambacho kitaongeza tija.
“Ninaamini kuwa mbali na maeneo hayo, viwanda vingine vingi vinaweza kuendelezwa kama vya usindikaji mazao ya kilimo na uzalishaji ,” alisema.
Alisema kwa upande wa Serikali mshahara wenye nafuu ya maisha kwa watumishi wake unapaswa kujengewa mazingira labda kwa kuweka idara maalumu ambayo inaangalia viwango vya mishahara.
“Kwa ilivyo sasa ni wazi kuna watumishi ambao wananufaika kama alivyowahi kueleza Rais. Yaani watu wanalipwa mishahara kama wapo Ulaya. Sasa mfano unaweza kukuta mtu kaajiriwa hapa UDSM ni msomi kwa viwango, lakini analipwa Sh3 milioni wakati mwenye digrii aliye Benki Kuu analipwa Sh6 milioni,” alisema.
Profesa Moshi alihoji kwa viwango hivyo viwili tofauti, nini kimetumika kuamua mwenye elimu kubwa alipwe kidogo na mwenye elimu ndogo alipwe zaidi.
Alisisitiza kuwa Serikali inapaswa kuzibana bodi za taasisi zake ambazo zimejijengea mazingira ya kulipa mishahara ya mamilioni ya fedha bila kujali hali ya nchi kwa ujumla.
Msomi mwingine, Dk Ulingeta Mbamba kutoka Shule ya Biashara ya UDSM, alisema Serikali inabidi idhibiti mfumuko wa bei.
“Ni wazi kwamba hata kama Serikali itaongeza mshahara, bidhaa zikawa zinapandishwa kiholela, hakuna siku kiwango cha mshahara kinaweza kutosheleza maisha ya watumishi,” alisema.
Post a Comment