Loading...

Uhaba-wa-madawati-wamtesa-RC-Iringa


Agizo la Rais John Magufuli la kutaka ifikapo Juni 30, mwaka huu kusiwe na wanafunzi wanaokaa sakafuni limeanza kumtesa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza baada ya kubaini upungufu wa madawati 37,412 huku tarehe ya mwisho ikikaribia.
Awali, Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wapya wa mikoa kuhakikisha wanabuni njia za kuondokana na tatizo hilo ifikapo tarehe hiyo.
Akizungumza na wadau wa elimu wa mkoa huo waishio Dar es Salaam walioahidi kuchangia madawati 510 yenye thamani ya Sh25 milioni, Masenza alisema upungufu huo unatokana na idadi kubwa ya wanafunzi walioandikisha darasa la kwanza na awali mwaka huu.
Alisema ni aibu kwa Iringa kuwa na wanafunzi wanaokaa chini kwa kukosa madawati na kuwataka wananchi kusaidia kuondokana na tatizo hilo ili kuwanusuru wanafunzi hao.
“Ikifika Juni 30, tusiwe na watoto wanaokaa chini hivyo nawaomba tusaidiane kuhakikisha madawati yanapatikana, naamini inawezekana,” alisema Masenza.
Ili kufanikisha azma hiyo, alisema amekubaliana na viongozi wakiwamo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na katibu tawala wa mkoa huo kuchangia madawati 20 kila mmoja kutoka mifukoni mwao.
Alisema katibu tarafa atachangia madawati matano, watendaji kata matatu na kila ofisa mtendaji wa kijiji au mtaa dawati moja.
Masenza alisema jumla ya wanafunzi 65,955 wameandikishwa darasa la kwanza na awali mwaka huu idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Alisema mkoa huo una madawati 126,286 kati ya 163,698 yanayohitajika huku kukiwa na upungufu wa madawati 25,865 kwa shule za msingi na awali.
Alisema katika shule za sekondari yanahitajika madawati 11,547.
Masenza alisema ongezeko la wanafunzi linadhihirisha kuwa wapo watoto waliokuwa wakikosa elimu kutokana na wazazi wao kukosa fedha kwa ajili ya kuwasomesha.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayoub alisema mkakati wao ni kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa manufaa ya wakazi ikiwamo kumaliza tatizo la madawati.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera alisema zimeundwa kamati tatu kwenye mkoa huo kwa ajili ya shughuli ya uchagiaji wa madawati.
Wadau wa maendeleo mkoani Iringa wanaoishi Dar es Salaam, walisema wapo tayari kuchangia maendeleo endapo watakuwa wakishirikishwa

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright NEWZ | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top