VIJANA wamegoma kujitokeza na kushiriki uchaguzi wa marudio visiweani Zanzibar na kusababisha zoezi hilo kuzorota, anaandika Mwandishi Wetu.
Katika mitaa mbalimbali Unguja na Pemba kuna hali ya utulivu huku maofisa usalama wakitembea maeno mbalimbali kuangalia hali ya usalama.
Kwenye uchaguzi huo, wanaojitokeza kwenda kupiga kura ni watu wazima wanawake na wanaume ambapo vijana wa kike na wa kiume wanaonekana kupuuza uchaguzi huo.
Hatua hiyo inaelezwa imechagizwa na msukumo wa chama kikuu cha upinzani visiwani humo-Chama cha Wananchi (CUF) kilichogomea kushiriki uchaguzi huo.
Hali ni mbaya zaidi katika Kisiwa cha Pemba ambapo wasimamizi wa vituo vya uchaguzi wengine wamelazimika kusinzia kutokana na wapiga kura kwenda mmoja mmoja baada ya muda mrefu kupita.
Uchache wa wapiga kura unathibitishwa na kauli ya Hamad Rashid, Mgombea Urais Kupitia Chama cha ADC kwamba, watu ni wachache kulinganisha na uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana.
Hamad alifika kupiga kura kwenye Kituo cha Tondooni Wawi wilayani Chake-Chake, Mkoa wa Kusini Pemba akisema ‘hali ndivyo ilivyo’ na kwamba watu ni wachache.
Hata hivyo, amelalamikia hatua ya vyama kutoshiriki uchaguzi huo akidai kwamba, hakukuwa na sababu ya wao kujitoa kwa kuwa sheria iliwataka kwenda mahakamani kuapa kutoshiriki uchaguzi huo.
Kwenye vituo vingi, Pemba wasimamizi wanasubiri wapiga kura huku maofisa wa usalama wakiwepo vituoni hapo.
Miongoni mwa vituo vilivyochelewa kupata wapiga kura leo licha ya kufunguliwa mapema ni Kituo cha Madungu Chake-Chake, Pemba.
Miongoni mwa wapigakura waliojitokeza mapema kwenye Kituo cha Kupigia Kura cha Bungi, Kibera Unguja ni Dk. Ali Mohammed Shein, Mgombea wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye alifika kituoni hapo majira ya saa 1:08 asubuhi.
Hali ya wasiwasi bado ipo miongoni mwa Wanzibari kutokana na kutojua hatma ya Zanzibar.
Ni baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Serikali ya CCM kulazimsha marudio ya uchaguzi huo baada ya ule wa Oktoba 25 mwaka jana unaotajwa CUF kuibuka mshindi na matokeo hayo kufutwa.
Post a Comment