ISAYA Mwita Charles, mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameshinda Umeya wa Jiji la Dar es Salaam, anaandika Hapyyness Lidwino.
Kwenye uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Sara Yohana, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji amemtangaza Charles kuwa mshindi kwa kupata kura 84 dhidi ya Yusuph Omary Charles wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 67.
Akitangaza matokeo hayo Sara amesema, kura zilizopigwa kwenye uchaguzi huo ni 158 ambapo kura halali zilikua 151 na zilizoharibika ni saba.
Katika uchaguzi huo, mgombea wa Chadema (Charles) ameungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Dar es Salaam, vyama hivyo ni ni Chadema yenyewe na Chama cha Wananchi (CUF).
Uchaguzi huo umehudhuriwa na wanachama pia viongozi mbalimbali wa Ukawa, miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema- Taifa na Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema na kuungwa mkono na Ukawa.
Kufanyika kwa uchaguzi huo kumetatua mvutano wa muda mrefu uliokuwepo kati CCM na Ukawa na kusababisha uchaguzi huo kuahirishwa mara tatu huku baadhi ya wabunge na madiwani wa Ukawa Dar es Slaam kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujeruhi.
Post a Comment