Loading...

ZANZIBAR SASA CHINI YA MTUTU WA BUNDUKI

Askari wakilinda amani mitaa ya Zanzibar
SERIKALI ya Umoja wa Kitaifa (SUK) katika Visiwa vya Zanzibar imefikia tamati, anaandika Yusuph Katimba.
Uchambuzi wa kisheria unaonesha kuwa utawala wa sasa wa Zanzibar haufuati katiba, na kwamba hata kama ingefuatwa, haiwezekani tena kuwa na SUK, kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyojengwa kati ya tarehe 25 Oktoba 2015 na 20 Machi 2016.
Tundu Lissu, wakili wa mahakama kuu, anaamini kwamba Zanzibar sasa hivi inatawaliwa kwa mtutu badala ya katiba; akiungwa mkono na Awadhi Ali Said, Wakili wa Mahakama Kuuu Zanzibar.
Lissu anasema: “Hakuna hoja ya kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwa kuwa serikali haifuati katiba. Hakuna jambo lolote Zanzibar linalofanywa kwa kufuata Katiba, Zanzibar inaendeshwa kwa mtutu wa bunduki.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni ya Chama Cha Mapinduzi na Chama cha Wananchi – CUF, na wala si ya ADC na vyama vingine vinavyosindikiza.
“CCM na haiwezi kufuata lolote kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Inafanya namna inavyoweza. Kama serikali ingekuwa inafuata katiba basi Maalim Seif (Maalim Seif Sharif Hamad) angekuwa Rais wa Zanzibar.
“Haiwezekani kuwepo kwa serikali hiyo kwa kuwa uchaguzi huo (wa 20 Machi 2016) ulikuwa haramu, uliitishwa na tume haramu, chini ya serikali haramu.
“Hakuna kitu kinachoitwa Serikali ya Umoja. Tume haramu, uchaguzi haramu, na ulisimamiwa na serikali haramu. Chochote kinachofanywa kwa sasa ni haramu.”
Naye Said anasema katiba inaelekeza kuwa lazima chama kitakachoingia kwenye serikali kiwe na asilimia kuanzia 10 na kuendelea.
“Kama hakuna chama kilichofikisha asilimia hizo, basi chama cha pili chenye wawakilishi wengi wa majimbo ndio kitakachotoa makamu wa kwanza wa rais.
“Sasa hapa utawezaje kuunda serikali ya umoja wa kitaifa? Kama serikali inayoundwa itaachana na vyama vingine hakutakuwa na serikali ya namna hiyo,” amesema.
Kuhusu hoja kama itabidi serikali ya sasa ibadili katiba ili kufuta rasmi SUK, anasema: “kubadilisha katiba nako hakuwezi kufanikiwa kwa kuwa serikali haijakamilika. Hakuna Makamu wa Kwanza wa Rais anayekubalika kwa Katiba ya Zanzibar. Maana yake ni kwamba huwezi kupeleka muswada katika Baraza la Wawakilishi ili baadaye iitishwe kura ya maoni.”
Anasema uchaguzi wa marudio Zanzibar haukukidhi matakwa ya katiba ya Zanzibar, kwa hiyo kila kinachofanywa na serikali ya sasa ni batili.
Zanzibar imeingia katika mgogoro mpya wa kisiasa tangu 28 Oktoba 2015, baada ya Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi ambayo yalikuwa yanaelekea kumpa ushindi Maalim Seif Sharrif Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF).
Jecha hakuwa na mamlaka ya kikatiba kufuta uchaguzi huo, na taarifa zinasema alishurutishwa na vyombo vya dola vilivyoamriwa na Dk. Ali Mohamed Shein, aliyekuwa anagombea tena kiti hicho akiwa rais.
Hatimaye, Jecha alitangaza kuwa uchaguzi huo ungefanyika tarehe 20 Machi 2016. CUF kilisusia uchaguzi huo, kukafanyika uchaguzi wa upande mmoja ulioshirikisha CCM na vyama vidogo vilivyo upande wa CCM na visivyo na wafuasi Zanzibar, chini ya ulinzi mkali wa majeshi.
Katika matokeo ya uchaguzi huo wenye utata, Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM alitangazwa mshindi kwa kupata kura 299,982 (91.4%) akifuatiwa na Hamad Rashid Mohamed wa ADC kwa kura 9,734 (3.0%).
Katiba ya Zanzibar inasema akishapatikana rais, anayemfuata kwa kura, iwapo atakuwa amefikisha walau asilimia 10 ya kura, ndiye atakuwa makamu wa kwanza wa rais, akitoka chama cha upinzani.
Katika uchaguzi wa Machi 20 hakuna mgombea aliyefikisha asilimia 10. Hivyo, kikatiba, haitawezekana kumpata makamu wa kwanza wa rais kutoka upinzani; na hivyo SUK itakuwa imefikia tamati.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright NEWZ | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top