Loading...

TAKUKURU Yaanza Kuchunguza "Mabilioni ya JK"

 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeanza kuchunguza fedha za uwezeshaji maarufu kama ‘Mabilioni ya JK’ ambazo hazikurejeshwa na wakopaji nchi nzima. 

Msemaji wa Takukuru, Tunu Mleli alisema jana kuwa taasisi hiyo imechukua jukumu hilo kwa sababu moja ya majukumu yake ni kuchunguza masuala ya rushwa na kutoa rai kwa mtu mwenye ushahidi au taarifa kuhusu suala hilo kuzitoa kwa taasisi hiyo. 


“Takukuru ipo wazi kuzipokea taarifa hizo ili zitusaidie kwenye uchunguzi,” alisema Tunu. 


Kati ya Sh50 bilioni zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, ni Sh43 bilioni tu zilizorejeshwa, huku Sh7 bilioni zikidaiwa kutafunwa. 


Fedha hizo zilitolewa na Kikwete kwa ajili ya kuwawezesha kimitaji, wajasiriamali nchi nzima, mikopo ambayo ilipitia benki za CRDB, NMB, Community Bank na Benki ya Posta Tanzania. 

Fedha hizo kutoka Mfuko wa Rais, zilikuwa zikikopeshwa kwa riba ya asilimia 10, ambapo asilimia mbili ilikuwa inaingia serikalini na nane ilikuwa inabaki kwenye benki hizo. 


Hata hivyo, baadhi ya vyama vya Akiba vya Kuweka na Kukopa (Saccos), vilivyopewa fedha hizo, vilitoa mikopo hiyo kiholela, huku baadhi ya viongozi wakidaiwa kutengeneza majina feki na kukopeshana fedha hizo. 


Imedaiwa kuwa Saccos nyingi ambazo zilifuja fedha hizo katika mikoa mbalimbali, viongozi wake wengi walikuwa pia ni viongozi wa kisiasa na wengine wakiwa na nyadhifa serikalini. 


Kwa mujibu wa uchunguzi huo, baadhi ya waliokopeshwa fedha hizo na Saccos mbalimbali, hawakuwa wanachama, bali walichomekwa baada ya kuonekana kuna fursa ya ‘kupiga dili’. 


Chanzo kutoka Takukuru, kimedokeza kuwa makamanda wa taasisi hiyo katika mikoa mbalimbali, wamepewa maelekezo ya kuchunguza mahali yalipo mabilioni hayo na nani waliyafuja. 


“Ni kweli tumepewa maelekezo ya kuchunguza fedha hizo. Unajua hizi ni fedha za umma haziwezi kutafunwa tu hivihivi na Serikali ikakaa kimya,” alidokeza mmoja wa maofisa wa Takukuru. 

Machi mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Christopher Chiza aliagiza kufanyika kwa ukaguzi wa kina wa fedha hizo. 


Alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake katika Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (Neec), ambako aliagiza watakaobanika kuhusika na ubadhirifu wa fedha hizo wachukuliwe hatua za kisheria. 


“Lazima tuangalie mabilioni ya JK yalipotelea wapi, yalivyofujwa na wahusika wapo wapi ili sheria ichukue mkondo wake. Nimeambiwa kuna zilizobaki tujue ziko wapi,” alikaririwa Chiza akisema. 

Lakini Desemba 24, 2013, mtangulizi wa Chiza, Mary Nagu alikaririwa akisema Sh43 bilioni kati ya Sh50 bilioni za mabilioni ya JK zilizokopeshwa kwa wajasiriamali 74,701 zilikuwa zimerejeshwa. 


Nagu alitoa takwimu hizo alipokuwa akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Rais Kikwete katika, utaratibu uliofanywa pia na wizara nyingine. 

Suala la mabilioni hayo ya JK limekuwa likiibuka mara kwa mara bungeni na katika mitandao mbalimbali ya kijamii huku wananchi wakitaka zirejeshwe. 
Via>>Mpekuzihuru.com

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright NEWZ | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top