Kuhusika na uuzwaji wa mgodi wa Tanzanite One ulioko Mererani wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa kampuni ya kigeni ya Sky Associate.
Mallya aliyasema hayo jana bungeni mjini Dodoma, wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini akieleza huenda mawaziri hao wanahusika na uuzwaji wa kampuni hiyo, huku akimhusisha Jenista kuwa na undugu na Yusuph Mhagama aliyemuoa mmoja wa viongozi wa kampuni hiyo aitwaye Asia Gonga.
Millya alisema hata zabuni ya uuzwaji wa Mgodi huo haikutangazwa kwani kampuni hiyo ya mfukoni ilitengenezewa kwa ajili ya ulaji na baadhi ya mawaziri ambao ni Simbachawene ambaye kwa wakati huo alikuwa Waziri wa Nishati na Madini na hakutangaza zabuni.
Alisema Jenista Mhagama anahusika katika uuzwaji wa Mgodi huo kwa sababu mmoja wa viongozi wa juu wa kampuni hiyo iliyonunua Mgodi huo (Sky Associate) anaitwa Mhagama na inadaiwa ni shemeji yake.
“ Kwa bahati mbaya mheshimiwa Mwenyekiti mama yetu Mhagama ametajwa kuwa shemeji wa mmoja wa mbia wa hapo dada anaitwa Asia Gonga ambaye ameolewa na Yusuph Mhagama,”alisema Miilya.
Mara baada ya Millya kumtaja Jenista Mhagama, ghafla Waziri huyo aliomba taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge na alisema majina ya Mhagama yapo mengi na ni ukoo mkubwa na kwamba hana uhusiano wowote na majina yaliyotajwa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kumpa taarifa mbunge aliyekuwa anazungumza kuwa katika nchi hii jina Mhagama ni kubwa na ukoo wangu hauna mtu anayemtaja, anachokisema si sahihi na hakikubaliki na asiendelee kuchafua ukoo wetu kwa sababu majina yanafanana bila yeye kufanya utafiti,”alisema Mhagama.
Dakika chache baada ya Jenista kutoa taarifa ,Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga, alimuuliza Millya endapo amepokea taarifa hiyo, lakini alisema ‘Jenista amekiri mwenyewe kuwa ukoo wao ni mkubwa na jina hilo linatajwa katika mgodi huo huku akisisitiza kuwa kutakuwa kuna dili limecheze hapo.
“Mheshimiwa mwenyekiti nimesema taarifa tuu na Jenista alipaswa kusema kuwa hahusiki na mtu aliyetajwa na si mambo mengine, kama wachimbaji hawasaidiwi na Wizara ya Kazi ambayo ipo chini yake kwanini asihusishwe kwenye suala hilo?,”alihoji Millya.
Mara baada ya majibizano hayo, Millya aliendelea kuchangia na alisema serikali ni mbia na Stamico na mgodi huo uliuzwa kiholela na kuiomba serikali ieleze ulipatikanaje na uliuzwaje kwa kampuni ya Sky Associate na zabuni hiyo ilitangazwa lini na wapi.
“Imekuwaje Simbachawene asaini mkataba ili kampuni iingie kwenye ubia na serikali lakini hakuna mtu aliyeshindana naye?..eti walitangaza kule kwenye soko la hisa la Uingereza je ni watanzania wangapi wangeona au wenye uwezo wa kuona…. .leo wachimbaji wadogo wananyanyaswa kwenye mkataba huo hadi wengine wanapoteza maisha,”alisema Millya.
Hata hivyo, Millya alimwomba Waziri Muhongo kuunda tume kwa ajili ya kuifuatilia kampuni hiyo na suala hilo kwa kuwanyanyasa wananchi wa Simanjiro.
Alisema madini yanaibiwa kila siku na kampuni hiyo na kuongeza kuwa iliwahi kuwafukuza wafanyakazi wapatao 201 na kuwapeleka mahakamani bila ya kuwalipa mafao yao.
Hata hivyo, baada ya Millya kumaliza kuchangia, Jenista aliomba mwongozo wa Mwenyekiti na alipopewa nafasi alieleza kuwa wabunge wamekuwa na tabia ya kuchafua majina ya mawaziri bila kuchukuliwa hatua hivyo aliomba mwongozo wa kumtaka mbunge huyo kutoa ushahidi wa alichokizungumza au afute kauli yake.
Post a Comment