Loading...

Naibu Waziri Ajibu swali Lililomponza Kitwanga.....Asema Serikali Imekusudia Kujenga Nyumba 9500 Kwa Ajili Ya Askari Magereza



Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusufu amejibu upya swali lililomponza bosi wake wa zamani, Charles Kitwanga.

Uamuzi wa kurudia swali hilo ulitolewa juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisema swali hilo lilijibiwa katika hali ya ulevi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na wabunge wakaomba mwongozo kuhusu majibu yaliyotolewa.

Kitwanga aliondolewa katika nafasi yake na Rais John Magufuli baada ya kujibu ya swali hilo akiwa amelewa.

Leo, Masauni amejibu swali hilo namba 211 la Mbunge wa Viti Maalumu Devota Minja (Chadema) na kuonyesha utofauti mkubwa kati ya majibu yake na yale yaliyotolewa mwishoni mwa wiki na aliyekuwa Waziri wake.

Swali hilo ambalo awali lilikuwa namba 205, liliulizwa na Devota Minja akitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuboresha makazi ya polisi na askari magereza wanaoishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi ukilinganisha na kazi zao kwa jamii.

Nyakati zote hizo, swali hilo limeulizwa na wabunge tofauti wa Chadema kutokana na Minja kutokuwapo, mara ya kwanza likiulizwa na Suzan Kiwanga (Mlimba) na leo Joseph Selasini wa Jimbo la Rombo.

Tofauti ya majibu ya Kitwanga, Masauni ametoa takwimu katika ujenzi wa nyumba 9,500 za Magereza nchi nzima ambapo amesema  tayari serikali imekwisha ingia mkataba na Kampuni ya Poly Technologies ya China kujenga nyumba hizo.

Mhe. Masauni alibainisha kuwa  kupitia mkataba huo Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto iliyopo ya uhaba wa nyumba kwa ajili ya askari wa jeshi hilo ambapo mahitaji kwa sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni nyumba 4,221 hivyo kupelekea upungufu wa nyumba 10,279.

“Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na Polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi, hivyo katika kukabiliana na tatizo hili Serikali imeendelea kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba na pia kujenga nyumba mpya”. Alisema Masauni.

Mhe. Masauni alifafanua  kuwa mgawanyo wa ujenzi wa nyumba hizo mpya ni Makao Makuu ya Magereza nyumba 472, Arusha nyumba 377, Dar es Salaam nyumba 952, Dodoma 356, Kagera 364, Kigoma 272, Kilimanjaro 390, Lindi 233, Manyara 206, Mara 378, Mbeya 622, Iringa 336, Morogoro 669, Mtwara 215, Mwanza 398, Pwani 384, Rukwa 358, Ruvuma 320, Shinyanga 337, Singida 299, Tabora 408, Tanga 382, KMKGM Dar es Salaam 219, Chuo cha Ukonga 115, Chuo cha Kiwira 183, Chuo cha Ruanda 62, Chuo KPF 27, Bohari Kuu 82 na Bwawani nyumba 84.

Aidha, Mhe. Masauni aliongeza kuwa kwa upande wa Jeshi la Polisi, Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar zitakazosaidia kupunguza tatizo la makazi kwa askari wa jeshi hilo.

Mhe. Masauni alilieleza bunge kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri hali ya uchumi itakavyokuwa inaimarika.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright NEWZ | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top