KWA hakika mambo yanayofanywa na Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar ni aibu tupu. Maisha ya Wazanzibari yamepoteza mwelekeo sababu kuu ni mkakati wa jeshi hilo kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushika nchi, anaandika Hapyness Lidwino.
Maisha ya wasiwasi yanashika kasi, wananchi wanaishi kwa hofu huku, wanateswa na wengine wanakamatwa na kuswekwa ndani kwa kuwa wanaonesha kutoridhika na harakati za jeshi hilo na CCM.
Hata wale ambao si wafuasi wa vyama vya siasa visiwani humo wanakiona cha mtemakuni, nchi inaendeshwa kimabavu. Wenye hofu zaidi wanatoroka Pemba.
“Yanayofanyika hapa yanaweza kukutoa machozi, unyama wanaofanyiwa raia hauna kipimo, yaliyoelezwa na CUF kuhusu kipigo ni kweli,” anazungumza raia mmoja wa Zanzibar ambaye ameomba kuhifadhiwa jina lake na kuongeza;
“Yanayofanyika Zanzibar yanafichwa na yanapaswa kufichwa na watawala kwa kuwa ni aibu, ni aibu wallah. Kila mpenda amani hawezi kuvumilia, ni lazima atoe machozi yake, hatuna raha hatuna amani.”
Zanzibar imeingia kwenye utata zaidi baada ya Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta kinyume cha sheria matokeo ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo tarehe 28 Oktoba mwaka jana.
Yanayotokea visiwani Zanzibar kwa sasa yalionywa na wasomi, wanaharakati, viongozi wa dini, mataifa ya nje na wanahabari.
Kumbukumbu ya Gazeti la MAWIO lililofutwa na serikali tarehe 15 Januari mwaka huu liliandika kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Z’bar’ ambapo ndio sababu ya kufutwa kwake. Yanayotokea sasa yanaakisi kilichoandikwa na MAWIO.
Uchaguzi huo uliopangwa kufanyika kesho umeharibu mwelekeo wa maisha ya Wazanzibar kwa ujumla, wanaoumia ni wafuasi wa vyama na wasio wafuasi.
Kauli tata zimekuwa zikipazwa visiwani Zanzibar ikiwa ni kilele cha kuonesha kuwepo kwa wasiwasi, matukio mbalimbali yameakisi kuwa Zanzibar si salama.
Miongoni mwayo ni ile kauli ya wananchi wa Pemba kutakiwa kulala kabla ya saa tatu usiku. Kauli hiyo pia inawahusu wageni (watalii) ambao wametakiwa kurejea katika nyumba za wageni walimofikia kabla ya muda huo. Hakuna amani Zanzibar.
Jeshi la Polisi limekuwa likikamata wanachama wa Chama Cha Wananchi (CUF), wanavamia ofisi za chama hicho na kuharibu mali zao huku wakiwa na mitutu ya bunduki na vifaru vya vita. Usalama upo wapi?
Tayari wafuasi na viongozi wa CUF zaidi ya 60 wamekamatwa na polisi, miongoni mwao ni Eddy Liamy mwanamikakati ya ushindi CUF; Nassoro Mazrui, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar; Mahomoud Mahinda, Katibu Mtendaji JUVICUF; Abeid Hamis Bakari, Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi na Hamad Masoud, Mkurugenzi wa Habari CUF.
Mansoor Yusuph Himid, Mshauri Mkuu wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif amekamatwa kwa madai ya kuwa na taarifa za watu waliolipua maskani ya CCM iliyopo Kisongwe Michenzani Mjini Unguja.
Viongozi wa CCM wanaotoa kauli tata za kushawishi vurugu wanalindwa, ni Sadifa Juma Khamis, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVICCM) ambaye amawetaka vijana wa chama hicho kuwa tayari kwa mapambano.
Ofisi za CUF, CCM zachomwa moto, wanaokamatwa ni wanachama na wapenzi wa CUF pekee. Haki ipo wapi? Amani ipo wapi Zanzibar? Mataifa ya kimataifa yapo kimya.
Idadi ya wanajeshi imeongeza, hofu inatokana na nini? Nani anasakwa? Je hawana kazi nyingine? Kwanini Serikali ya CCM inatumia nguvu kutwaa mamlaka? Mazombi wanafumbiwa macho, raia wanakamatwa. Hii nini?
Shangaa hapa, Hamdan Omar Makame, Kamishna wa Polisi Zanzibar ananukuliwa ‘’sisi hatujawahi kuwaona hao masombi bali tunasikia tu katika vyombo vya habari.’ Hawa wanaokanwa wanatumia usafiri wa serikali. Zanzibar ni aibu.
CHANZO: MWANAHALISIONLINE:
CHANZO: MWANAHALISIONLINE:
Post a Comment