Mtwara. Madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Rufani Mkoa wa Mtwara, Ligula, wamegoma kutoa huduma baada ya mwenzao kudaiwa kupigwa na ndugu wa mgonjwa hadi kuvuliwa nguo.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 5.00 asubuhi, baada ya mgonjwa kulazwa hospitalini hapo tangu Jumamosi kutokana na ajali ya pikipiki na kupewa rufaa jambo lililowaudhi.
Madaktari wa hospitali hiyo walioshuhudia tukio hilo, walisema majeruhi alifikishwa hospitalini Jumamosi akiwa ameumia na aliendelea kupatiwa huduma.
Madaktari hao waliomba kutotajwa, walisema mwenzao alipigwa baada ya kutoa taarifa za rufaa kwa ndugu wa mgonjwa kuwa anatakiwa kupelekwa Muhimbili.
Daktari mwingine alipoulizwa sababu za wao kutotoa huduma na kujikusanya kwenye moja ya jengo la hospitali hiyo, alidai ni kwa ajili ya usalama wao kwani kitendo alichofanyiwa mwenzao kimewafedhehesha na kuwadhalilisha.
Mmoja wa wagonjwa walioathiriwa na mgomo huo, Zamda Kupwaja alisema alifika hospitalini hapo majira ya saa 6.00 mchana, alipata cheti na alipomuona daktari alimwandikia dawa alipokwenda dukani hapakuwa na mhudumu.
Daktari aliyepigwa, Saini Dickson alisema alikwenda kumuona mgonjwa kama kawaida kwani alishamwandikia vipimo (x-ray) na kwamba, alianza kupatiwa matibabu ya nyama kabla ya mfupa.
“Baada ya kuona vipimo, niliwaeleza nitawaandikia waende Muhimbili wakaanza kulalamika kwa nini isiwe Nyangao au Ndanda, nikawaambia sifahamu matibabu yao siwezi kumtoa mgonjwa hospitali ya rufaa nimpeleke ya chini,” alisema Dk Dickson.
Post a Comment