KATIKA siku za hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa ripoti inayoelezea kuwa, usingizi ni moja ya jambo muhimu na kutopatikana kwake kunaathiri zaidi afya ya mtu, anaandika Michael Sarungi.
Shirika hilo limeeleza kuwa, afya ni hali ya kustawi kimwili, kiakili na kijamii. Hii ina maana kuwa si suala la mwili kukosa maradhi pekee kama wengi wanavyoweza kufikiri.
Hivyo ndivyo ukweli ulivyo ingawa tatizo lililopo ni kwamba, wengi hawajui walale muda gani na kwa sababu zipi, wanatakiwa kulala kwa saa ngapi kwa siku ili waweze kutimiza matakwa ya afya kama inavyoshauriwa kiafya.
Hili ni tatizo kubwa duniani na linasumbua watu wengi. Kupungua kwa ufanisi katika utendani wa shughuli mbalimbali ni miongoni mwa sababu zinazohusishwa na kutolala vizuri.
Taasisi ya National Sleep Foundation ya Marekani, mwanzoni mwa Februari ilitoa ripoti mpya inayoainisha saa za kulala kulingana na umri wa kila mtu.
Ripoti hiyo imetokana na tafiti tofauti.
Kutokana na majibu ya utafiti huo mpya, sasa mtu anaweza kulala kwa muda unaofaa ili kuifanya afya iwe imara bila kujali kazi anayofanya, bali umri.
Ripoti hiyo ya kitaalamu iliyotolewa na jopo la wanasayansi na watafiti 18 kwa kupitia tafiti zaidi ya 300, inaonesha kuwa watu wanapaswa kulala zaidi tofauti na ripoti za awali zinavyoeleza.
Utafiti huo unaeleza kuwa watoto wachanga, wenye umri wa mwezi mmoja hadi miezi mitatu wanahitaji kulala kwa kati ya saa 14 mpaka 17. Wenye miezi minne mpaka 11 wanatakiwa kulala kwa saa kati ya 12 mpaka 15, wakati wale wenye mwaka mmoja na miwili wanahitaji saa 11 mpaka 14.
Wenye umri wa kusoma chekechea, ambao ni miaka mitatu hadi mitano, wanahitaji saa 10 mpaka 13, wakati wale wa shule za msingi, wa umri kati ya miaka sita hadi 13, wanahitaji kati ya saa tisa mpaka 11 za kulala.
Wanafunzi wa sekondari, wenye miaka kati ya 14 na 17, wanashauriwa kutumia muda wa saa nane hadi kumi. Wanafunzi wa vyuo, walio na umri wa miaka 18 mpaka 25, walale kwa kati ya saa saba hadi tisa.
Muda huo pia unashauriwa kwa watu wazima, kuanzia umri wa miaka 26 mpaka wazee wenye umri wa miaka 65 na kuendelea.
Muda huo unapendekezwa kwa watu wasio na dharura au wagonjwa. Katika hali kama hizo, muda unaweza kubadilika kulingana na mahitaji. Lakini haishauriwi kuzidisha saa mbili kwa watoto na saa moja kwa watu wazima.
Hata hivyo, kumbukumbu zinaonesha kuwa baadhi ya tafiti za awali ziliwahi kushauri tofauti. Mfano; Ripoti ya Taasisi ya Taifa ya Afya Marekani iliwahi kushauri kuwa, watoto wachanga walale kwa saa 16 mpaka 18, chekechea walale kwa saa 11 mpaka 12 na wale wa shule za msingi walale walau kwa saa 10.
Hali hii ya kutopata usingizi wa kutosha imekuwa na madhara ya kiafya kwa wananchi wengi katika nchi nyingi za Afrika kwa sababu za kiuchumi zinazowafanya kukosa muda na wa kutosha kulala.
Wakati mwingine dalili za mtu zinaweza kuonesha kwamba ana tatizo kubwa la usingizi. Kuna tatizo la kukosa usingizi ambalo hudumu kwa zaidi ya mwezi mmoja na mara nyingi huhusianishwa na magonjwa mengine makubwa, kama vile kushuka kwa mapigo ya moyo.
Ingawa tatizo hilo huwapata sana wanaume wanene kupita kiasi waliozidi umri wa miaka 40, linaweza pia kuwapata watu wenye umri wowote, hata watoto. Kuna matibabu mbalimbali na yote yanapaswa kutolewa na daktari wa matatizo ya usingizi.
Tatizo la kusinzia mchana huanza mtu anapokuwa na umri wa miaka 10 mpaka 30. Wakati mwingine watu wenye tatizo hilo huonekana kuwa timamu lakini hawatambui wakati ukipita.
Ubaya wa tatizo hilo ni kwamba, mara nyingi halitambuliwi kwa miaka mingi, huku mtu anayeugua akidhaniwa kuwa mvivu, kwamba anafikiri polepole, au anaonekana kuwa mtu asiyeeleweka.
Ugonjwa mwingine ni ule wa kusaga au kukaza meno sana wakati mtu anapolala. Ugonjwa huo unaweza kuharibu meno na kusababisha maumivu makali ya taya, hivyo mtu hushindwa kulala kabisa.
Kuna tiba mbalimbali kama vile upasuaji wa mdomo na kutumia kifaa cha kukinga meno usiku kwa kutegemea kiwango cha ugonjwa.
Mazungumzo haya mafupi kuhusu magonjwa kadhaa ya usingizi yanaonyesha kwamba ni hatari kuyapuuza. Huenda matibabu yakawa sahihi au tata, lakini mara nyingi ni ya lazima kwani inafaa kupata msaada wa kitiba haraka.
Post a Comment