PATRICK Asenga Diwani wa Kata ya Tabata (Chadema) ameshinda kesi ya uchaguzi aliyofunguliwa na Sudi Kasim aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, anaandika Faki Sosi.
Kasim alifungua kesi hiyo akipinga matokeo ya kiti hicho katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana kwa madai kwamba haukuwa huru na haki.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo leo katika Mahakama hiyo, Frank Moshi hakimu aliyekuwa akisikiliza shauri hilo amesema, anatupilia mbali kesi hiyo kwasababu mdai ameshindwa kuthibitisha malalamiko yake.
Miongoni mwa vitu alivyoshindwa kuthibitisha ni pamoja na uwepo wa vurugu katika kituo cha majumuisho ya kuhesabia kura ambapo hata wakala wake ameshindwa kuthibitisha hilo katika ushahidi wake.
Kutokana na hali hiyo, hakimu alisema kwamba uchaguzi ulikuwa huru na haki na kwamba Asenga ni diwani halali wa kata ya Tabata na atalipwa gharama ya 30 milioni kama fidia ya kesi hiyo.
Akizungumza nje ya mahakama, diwani Asenga amewashukuru wananchi wake kwa ushirikiano waliouonesha na kuahidi kuwa gharama za kesi atakazolipwa ataziingiza katika miradi ya maendeleo ya kata hiyo.
Amesema kuwa gharama hizo nakwamba atawasilisha madai ya fedha hizo mapema ili aweze kulipwa.
“Nashukuru wananchi wangu kwani nipo pamoja nao,mahakama imetenda haki.Hii kesi ilinipotezea muda wa kuwatumikia ,lakini kwasasa nipo huru na nipo tayari kuchapa kazi “amesema
Katika kesi hiyo,wadaiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ilala.
Katika kesi hiyo, Kasim aliiomba mahakama hiyo itenguwe matokeo ya uchaguzi kutokana na dosari mbalimbali zilizojitokeza na kwamba imtangaze yeye kama mshindi.
Post a Comment