Loading...

Dk. Shein, Maalim Seif wamyumbisha Mrema

Agustino Mrema, Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP)
AGUSTINO Mrema, Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) ‘amerusha mkuki msituni,’ ni baada ya kulalamikia wanasiasa wanaochochea uvunjifu wa amani visiwani Zanzibar bila kutaja majina yao, anaandika Aisha Amran.
Amelalamika kwamba, yeye na chama chake hawaridhiki na uchochezi huo na kuwawataka wananchi wa Zanzibar kudumisha umoja pia kupuuza kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaochochea vurugu.
Wanaoumana visiwani humo ni Maalim Seif Sariff hamad, aliyekuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kupitia Chama cha Wananchi (CUF) na Dk. Shein aliyegombea nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Taarifa za kushindwa kwa Dk. Shein kwenye uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana na baadaye Tume ya Uchaguzi Zanziabr (ZEC) kuilinda CCM kwa kuvunja Katiba ya visiwa hivyo, kumesababisha hali ya wasiwasiwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Jijini Dar es Salaam, Mrema aliogopa kutaja jina la mchochezi visiwani humo licha ya kujua mazingira yaliyompa ushindi Dk. Shein kwenye uchaguzi wa marudio uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu.
Mrema alilalama kuwa, kauli za viongozi wa siasa visiwani humo zinachochea kuvuruga amani hivyo wananchi wazipuuze kwani hakuna aliye juu ya sheria.
“Kuwepo kwa watu wanaochochea kuvuruga waangaliwe kama wahaini na hatua zichukuliwe dhidi yao katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama,” amesema Mrema.
Amesema mwaka 2001 Zanzibar iliingia katika machafuko yaliyopelekea watu kuuawa kutokana na vurugu za kisiasa, hivyo kutokana na historia hiyo wananchi wanatakiwa kuwa makini na kupuuza viongozi ambao bado wanaonekana kuwa na kauli za uchochezi.
“Hata nchi wahisani waache kuingilia mambo yetu ya ndani kwani wao hawaishi huku na hata mauaji yakitokea hawaguswi kwa lolote,” alisema Mrema
Mrema amesisitiza suala la uchochezi liangaliwe kwa macho mawili dhidi ya watu wanaotaka kuvuruga amani katika mazingira hayo, kwani Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC) haiangalii viongozi wa serikali na hata viongozi wa kisiasa ambao kwa namna moja wanakuwa wamehusika katika kusababisha mauaji kutokana na kauli wanazozitoa.
Mrema amekuwa tofauti na viongozi wengi wa vyama vya upinzani nchini ambao hueleza waziwazi kwamba, Dk. Shein na CCM wamepora ushindi wa Maalim Seif kwa kutumia mabavu wakisaidiwa na Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa ZEC kwa kuvunjwa kwa Katiba ya visiwa hivyo.
Miongoni mwa wanaonesha waziwazi kulalamikia ukandamizwaji wa demokrasia visiwani humo ni pamoja na Tundu Lissu, Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Tayari Chadema kimeungana CUF pamoja na Watanzania kulaani ukatili wa kisiasa uliofanywa na Serikali ya CCM visiwani humo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright NEWZ | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top