ianze kwa kusema asante Mungu kwa kila jambo ingawa machoni tuna furaha lakini mioyoni mwetu tumejeruhiwa vibaya sana. Ni wiki ngumu sana kwa maisha ya kawaida ya wafanyakazi wa Kampuni ya Global Publishers kwa kuondokewa na mfanyakazi mwenzetu, mwandishi hodari na muhimu kikazi, Makongoro Oging’.Tangulia mpendwa!
Wapo mamia ya watu waliofiwa na ndugu, jamaa, rafiki, wapenzi, wachumba, wake au waume zao, hakuna unafuu wa maumivu pindi mume au mke wako kipenzi anapotangulia mbele ya haki, ninaamini mwanaume akiachwa na mke wake hupata wakati mgumu sana kwa sababu ya kuwahudumia watoto kama baba na mama.
Vilevile baba anapotangulia, mama pia hupata wakati mgumu kwa sababu sasa anaanza maisha ya upweke, maisha ya yeye kusimama kama mama na baba. Na kama mwanamke hatakuwa imara basi atapata misukosuko ya hapa na pale.
Leo nazungumzia wake wa marehemu wanaoachwa baada ya wapendwa wao kutangulia mbele ya haki. Nafahamu ni kipindi kigumu sana ambacho wanawake wengi hukipitia pindi wanapoachwa na wapendwa wao ni ngumu kuamini kwamba umeachwa pekee yako, ni wakati mgumu kufikiria namna utakavyoitunza familia yako uliyoachiwa.
Ni wakati mgumu sana kufikiria ni namna gani utaendeleza mali kwa maana ya mashamba, nyumba na vitu vingine alivyoviacha mumeo.
Namuona namna mama, dada, shangazi na bibi yangu anavyohangaika na mateso ya kuachwa na mpenzi wake, mama hapati usingizi, hata uwezo wake wa kufikiri unafika kikomo hasa akiona watoto wake wanavyohitaji kwenda shule na yeye akiwa hawezi kujisimamia au kujiongoza.
Nikusihi mwanamke au mwanaume uliyeachwa na kipenzi chako, simama, nyanyuka tena, hakuna njia nyingine ya kuiona pepo isipokuwa kifo. Hivyo ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, yatupasa kufariki ili kuishi maisha ya milele kiimani.
Ni uchungu wa hali ya juu sana ambao pengine huwezi kuuelezea na ukaeleweka kwa mtu mwingine ambaye hajapata kukumbwa na janga hilo.
Yawezekana kuna kipindi unateswa na njozi kama vile unamuona mpenzi wako anakuita, anakuangalia na kukuonea huruma kwa unavyopambana na familia yenu, unaona anatamani kukuambia kitu lakini hana kauli. Kiukweli maumivu ya kufiwa yasikie kwa jirani yasikukute kwako au kwa mtu wako wa karibu.
Yote kwa yote muombee mumeo au mkeo kwa kumshukuru Mungu kwa kila jambo kwa kuwa yeye ndiye aliyemtoa na sasa amemtwaa. Maneno sahihi ya kutamka ni ‘Tangulia mpenzi wangu, mbele yako nyuma yangu’.
Kwa maoni, ushauri kuhusu mada usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta:mimi_na_uhusiano au jiunge kwenye group letu la WhatsApp kwa namba za hapo juu.
Post a Comment