Loading...
Home »
Unlabelled »
SERENGETI BOYS YAMALIZA MASHINDANO YA INDIA KWA HASIRA
TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ jana iliifunga Malaysia mabao 3-0 katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu kwenye michuano maalumu ya kimataifa nchini India.
Mchezo huo ulifanyika Uwanja wa Tilak, Maidan mjini Goa, India, ambapo kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Alfred Lucas hadi mapumziko Serengeti Boys ilishapata mabao hayo matatu.
Wafungaji walikuwa ni Makame Rashid dakika ya 14, Shaaban Add dakika ya 32 na Muhsin Makame dakika ya 45. Kwa mujibu wa Lucas, Serengeti Boys itarejea nchini leo saa moja usiku na kuwaomba wadau wa michezo kujitokeza Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kuwapokea.
Michuano hiyo iliandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la India, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka kesho.
Serengeti Boys ilimaliza hatua ya awali ikiwa na pointi sita sawa na Korea Kusini, lakini ikazidiwa bao moja hivyo kushika nafasi ya tatu katika michuano ambayo Marekani iliongoza kwa kufikisha pointi nane.
Kutokana na hali hiyo, Korea Kusini ikapata fursa ya kucheza na Marekani katika fainali jana jioni, huku Serengeti Boys ikicheza na Malaysia iliyoshika nafasi ya nne hatua za awali kutafuta mshindi wa tatu.
Thursday, 26 May 2016
Post a Comment