Baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Juliet Kairuki, mjadala umeibuka kuhusu kitendo cha mkurugenzi huyo mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kutochukua mshahara tangu mwaka 2013 alipoteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Kitendo hicho kimetajwa kuwa moja ya sababu za kutimuliwa kwake.
Swali hilo na sababu tofauti za uamuzi huo ndizo zilizotawala mijadala mbalimbali kwa siku nzima ya jana, ikiongozwa na mitandao ya kijamii.
Rais Magufuli alitangaza uamuzi wa kutengua uteuzi wa Kairuki Alhamisi ya jana akisema uamuzi huo ulifanywa tangu Aprili 24 na kwamba moja ya sababu za kuondolewa kwake ni kutochukua mshahara tangu Aprili, 2013.
“Pamoja na mambo mengine, hatua hii imechukuliwa baada ya Mheshimiwa Rais kupata taarifa kuwa Bibi Kairuki amekuwa hachukui mshahara wa Serikali tangu alipoajiriwa Aprili 2013 mpaka sasa, jambo linalozua maswali mengi,” inasema taarifa ya Profesa Adolf Mkenda, katibu mkuu wa Biashara na Uwekezaji wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Tofauti na watumishi wengine waandamizi ambao baada ya uteuzi wao kutenguliwa Ikulu ilisema watapangiwa kazi nyingine, kwa Kairuki atapangiwa kazi nyingine iwapo atataka kuendelea kufanya kazi serikalini.
Awali ilishawahi kuripotiwa katika vyombo vya habari kuwa Kairuki alikuwa hachukui mshahara uliotajwa kuwa Sh5 milioni (ambao Mwananchi haijaweza kuthibitisha) unaotolewa na TIC kwa kuwa ni mdogo kulinganisha na aliokuwa akipata nchini Afrika Kusini kabla ya kuombwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuja nchini kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.
Kabla ya kuteuliwa na Kikwete kushika nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Emmanuel Ole Naiko kustaafu, Kairuki alikuwa akifanya kazi Afrika Kusini katika chama cha benki cha Afrika Kusini, akiwa meneja mkuu wa Idara ya Benki na Huduma za Fedha.
Inadaiwa kuwa akiwa TIC, Kairuki, ambaye ni mwanasheria alikuwa akipendekeza apewe mshahara wa Sh18 milioni kwa mwezi kiwango ambacho kinadaiwa kingeendana na stahiki alizokuwa akipata Afrika Kusini. Madai hayo yalipingwa na Kairuki mwaka jana.
Katika mjadala mwingine, inaelezwa kuwa pamoja na kutolipwa mishahara, Kairuki aliweza kumudu maisha kutokana na kuwa na safari nyingi zinazoendana na nafasi yake ya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na hivyo kupata posho nzuri.
Kundi jingine lilieleza kwenye mijadala hiyo kuwa Kairuki alikuwa akilipwa posho zinazofikia Sh25 milioni na hivyo kuweza kumudu maisha bila ya kuchukua mshahara.
Hakuna mjadala ulioweza kuthibitisha madai hayo, lakini imeelezwa kwenye mitandao hiyo kuwa hali iligeuka baada ya Serikali kukubaliana naye mshahara na mtendaji huyo kudai malimbikizo yote ya mishahara ambayo hakulipwa.
Jitihada za kumpata Kariuki jana ziligonga mwamba.
Profesa Mkenda hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo la mshahara na mtumishi wake wa zamani.
“Mshahara wa nafasi hiyo upo na umekuwepo siku zote. Kabla yake kulikuwa na mtangulizi wake alikuwa anapokea mshahara,” alisema Profesa Mkenda kupitia ujumbe mfupi wa simu.
Alipoulizwa ni jambo gani lilitokea hadi Kairuki asichukue mshahara huo na Serikali ilichukua hatua gani za awali kumalizana naye mapema kabla ya kumalizika miaka mitatu, Profesa Mkenda hakujibu ujumbe wa swali hilo.
Lakini alisisitiza kuwa ngazi ya mshahara ya Mkurugenzi Mtendaji wa TIC ipo na haijawahi kubadilishwa tangu taasisi hiyo ianzishwe.
Hata hivyo, mwandishi wetu alipotaka ufafanuzi kutoka kwa katibu mkuu huyo iwapo mshahara ulikuwa ukiingia katika akaunti ya Kariuki halafu hautumii au haukupelekwa kabisa katika akaunti yake, hakujibu.
Katibu Mkuu Wizara ya Utumishi, Dk Laurian Ndumbaro alisema jambo hilo alikuwa amelisikia kwa mara ya kwanza mchana na kueleza kuwa Profesa Mkenda ana majibu zaidi.
Alipoombwa kuelezea iwapo kanuni au taratibu za utumishi zinambana mtu asiyechukua mshahara, aliahidi kumtafuta mwandishi kwa kuwa alikuwa bungeni lakini baadaye hakupokea tena simu.
Watu waliohojiwa na Mwananchi walikuwa na maoni tofauti.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Damian Shumbusho alisema iwapo alitenguliwa bila uchunguzi wa kina, uamuzi huo si wa busara.
Alisema kuwa iwapo kukubali kufanya kazi pasipo kuchukua mshahara ni kosa kwake na Serikali nayo inawajibika kwa kuwa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya Mwaka 2004 hairuhusu mtu kufanya kazi kabla ya makubaliano. “Hapa tatizo linaonekana lipo kwenye mkataba. Pasipo makubaliano ya mshahara mtu hawezi kufanya kazi,” alisema Shumbusho.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Nicholas Mgaya alionyesha wasiwasi wa mwajiriwa kutochukua mshahara.
“Unakula nini siku zote kama huchukui mshahara? Kwanini huchukui mshahara wako na kuutumia. Una kula rushwa au una chanzo kingine cha mapato kisichojulikana?” alihoji.
Alisema Tucta hawawezi kuzungumzia jambo lolote linalohusu wateule wa Rais kwa kuwa ana mamlaka kikatiba kutengua uteuzi wao, lakini wana uhakika Dk Magufuli alifanya uchunguzi wa kina na kushauriwa na wataalamu kabla ya hatua ya jana.
Mtaalamu wa masuala ya rasilimali watu, Elias Baraka kama wengine alihoji Kairuki alikuwa akiishi vipi bila kuchukua mshahara na kama uchunguzi umebaini hivyo ana tatizo la kukwepa uwazi.
“Kama uchunguzi umefanyika na ukabaini hivyo, ana kosa la kutokuwa mwaminifu. Hakuwa muwazi. Alikuwa anaishije bila mshahara? Hivyo adhabu hiyo itakuwa sahihi vinginevyo alitakiwa asimamishwe kwa uchunguzi zaidi,” alisema Baraka.
Wakati Profesa Mkenda akitangaza utenguzi huo, Kairuki alitakiwa kuwa mmoja wa waongozaji wa mkutano wa wawekezaji kutoka Urusi uliokuwa ukiendelea jana kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
Kairuki, ambaye taasisi yake ilikuwa moja ya waandaji wa mkutano huo, hakuonekana tangu asubuhi hata kabla ya tangazo la kutumbuliwa. Ratiba ya mkutano huo inaonyesha kuwa alitakiwa kuongoza mkutano huo muhimu sambamba na mwanzilishi wa kampuni ya b2b-export.com kutoka Urusi, Ekaterina Dyachenko na kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya Uendelezaji Biashara Tanzania (Tantrade), Edwin Rutageruka.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage a aliyekuwepo katika mkutano huo, alipoulizwa kuhusu sababu ya Kairuki kutopokea mshahara na sababu za Serikali kutochukua hatua kwa miaka aliyotumikia TIC, alisema hakuwa na taarifa za kutimuliwa kwa Kairuki.
“Hii ni habari (mpya) kwangu. Nimefika kutoka bungeni asubuhi hii,” alisema.
Post a Comment