Watu watatu akiwemo raia wa Kenya wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya aina ya Mirungi na Bangi kilo 54 na misokoto ya Bangi 4,500 ikisafirishwa kutoka nchini Kenya kwenda mkoani Arusha.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro Bw.Wilbrod Mutafungwa amesema watuhumiwa hao wamekamatwa katika maeneo ya njia panda Himo wilaya ya Moshi na Sanya juu wilaya ya Siha wakiwa wameficha madawa hayo ya kulevya kwenye miili yao kuanzia maeneo ya tumboni hadi miguuni.
Amewataja waliokamatwa ni Vitalis Victor mfanyabiashara mkoani Arusha, Naftal Mvoyi mkazi wa Voi nchini Kenya, Maulid Maulis mkazi wa Arusha ambao walikuwa wakisafirisha Mirungi kilo 44 kwa kutumia magazeti na gundi ya karatasi na kisha kuifunika kwenye nguo walizokuwa wamevaa wakitokea nchini Kenya kuelekea jiji la Arusha.
Ripota wetu amefanikiwa kuzungumza na baadhi ya vijana wanaojihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya katika manispaa ya Moshi na kueleza kwamba changamoto kubwa inayowabaili ni ukosefu wa ajira hali inayowasababisha baadhi yao kujihusisha na matukio ya uhalifu.
Matumizi ya madawa ya kulevya yameathiri vijana wengi kiafya kutokana na baadhi yao kushindwa kufanya shughuli za maendeleo na hivyo kulazimika kujihusisha na matukio ya wizi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Post a Comment