Mvutano mkali umeendelea kulikumba bunge la Afrika Kusini ikiwa siku moja baada ya wabunge wa upinzani kuzusha fujo kwa lengo la kuzuia hotuba ya Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo.
Katika vurugu hizo, maofisa wa kusimamia usalama bungeni waliwatoa nje kwa nguvu wabunge wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters kinachoongozwa na Julius Malema ambaye anatajwa kuwa kinara wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Rais Zuma.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa nje, Malema alisema Rais Zuma amepoteza haiba na dira ya kuwa kiongozi wa nchi hiyo na kwa msingi huo, hawatamruhusu alihutubie bunge hilo kwa amani.
“Zuma hatawahi kupata amani katika Bunge hili, hatuwezi kuongozwa na mtu ambaye ameshindwa kutii, kutetea na kulinda katiba ya nchi,” alisema.
Wabunge hao wamesisitiza kuwa wataendelea kupinga hatua yoyote ya Rais Zuma kuingia bungeni wakisema kuwa kiongozi huyo anapaswa kuachia madaraka kutokana na kukumbwa na kashfa mbalimbali. Tukio hilo la juzi ni la pili kuwahusisha wabunge hao wa upinzani na askari.
Itakumbukwa kuwa, mapema mwezi huu, wabunge wa upinzani walizusha vurumai bungeni kwa shabaha ya kuzuia hotuba ya Rais Jacob Zuma juu ya bajeti.
Katika vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya dakika 10, askari wa kutuliza ghasia waliamuliwa kuingia ndani na kuanza kuwaondosha kwa nguvu wabunge hao.
Wabunge hao walikuwa wakipinga hatua ya Rais Zuma kulihutubua bunge wakati akikabiliwa na kashfa ya matumizi mabaya ya madaraka. Naibu Rais wa chama hicho, Floyd Shivambu aliliambia bunge hilo wabunge wa upinzani hawako tayari kumwona Rais Zuma akiendelea kulihutubia bunge kama vile hakuna chochote kilichofanyika.
“Hatuwezi kumruhusu rais anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi kuhutubia taifa kana kwamba hakuna chochote kilichofanyika,” alisema.
Wapinzani nchini Afrika Kusini wanamtuhumu Rais Zuma kuwa ni kiongozi fisadi, baada ya Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo kumpata na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mahakama hiyo ilimuagiaza kulipa sehemu ya fedha zilizotumiwa katika ukarabati wa nyumba yake binafsi katika eneo la KwaZulu Natal, mradi ambao uligharimu zaidi ya Dola 16 milioni za Marekani.
Hata hivyo, Rais Zuma alinusurika kura ya kutokuwa na imani naye bungeni kufuatia kashfa hiyo
Post a Comment