Loading...

BUNGE LA BAJETI MCHAKAMCHAKA

Dodoma/Dar. Bunge la Bajeti ya Serikali ya 2015/16 linaanza leo mjini Dodoma kwa mwendo wa mchakamchaka kutokana na kuongezwa saa mbili kila siku ili limalizike Juni 27.
Saa za mjadala katika vikao zimeongezwa ili kuziba pengo la siku 12 zinazopungua na kutoa fursa kwa wabunge kuchangia bajeti za wizara na Bajeti Kuu ya Serikali ndani ya siku 44 ikilinganishwa na siku 56 zilizotumika kupitisha bajeti ya mwaka 2014/15 na miaka ya nyuma.
Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wa bajeti, wachumi na wanasiasa wamesema hawatarajii kuona jipya isipokuwa mipasho inayolenga Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Serikali imepanga kukusanya na kutumia Sh22.4 trilioni katika mwaka wa fedha 2015/16 ikiwa ni nyongeza ya Sh2.6 trilioni ikilinganishwa na Bajeti ya mwaka 2014/15 ambayo ilikuwa Sh19.8 trilioni.
Kwa miaka iliyopita, baadhi ya wizara zenye majukumu mengi zilikuwa zinatengewa siku mbili au tatu, lakini safari hii hali itakuwa tofauti kwa kuwa zitajadiliwa kwa siku moja tu au mbili kulingana na mjadala utakavyokuwa na mapumziko yatakuwa Jumapili pekee.
Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka alisema badala ya Bunge kuanza saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.00 mchana na baadaye saa 11 jioni hadi saa 1.45 usiku; sasa litaanza 3.00 asubuhi hadi saa 8.00 mchana na kuendelea saa 10.00 jioni hadi saa 2.00 usiku.
“Ili kuendana na muda, tumeongeza saa kadhaa ili kumaliza shughuli zote zilizopangwa. Siku za Jumamosi zitahesabika kama siku za kazi kama kawaida.” alisema.
Alisema Bunge hilo litamalizika Juni 27 lakini akaongeza: “Tumeacha siku tatu za dharura, kuanzia Juni 28 hadi 30 ili kama kuna jambo lolote la muhimu litajitokeza Bunge linaweza kuendelea kwa muda huo wa siku tatu.”
Alisema kutokana na mabadiliko ya uwasilishaji, ni lazima bajeti iwe imesomwa kabla ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka unaofuata Julai Mosi.
“Inawezekana tukapata kiongozi wa kulihutubia Bunge au katika upitishaji wa bajeti za wizara akidi isitimie na kulazimika shughuli husika kuendelea siku inayofuata. Zamani Bunge la Bajeti lilikuwa likianza Juni hadi Agosti, lakini kwa mabadiliko haya sasa lazima limalizike Juni,” alisema.
Alisema bajeti zote za wizara hadi kufikia Juni 10 zitakuwa zimeshasomwa, Juni 11 itasomwa Bajeti Kuu ya Serikali na kuanza kujadiliwa.
Alisema ratiba hiyo pia inaweza kuvurugika utakapoanza mfungo wa Ramadhani.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright NEWZ | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top