SIKU moja baada ya rungu la Rais Dk. John Magufuli, kumwangukia Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne-Kilango Malecela, aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amesema kinachofanyika sasa, siyo mwarobaini ni vigumu kukosekana watumishi hewa kwa mfumo uliopo.
Utouh ambaye amehudumu kwenye nafasi ya CAG kwa miaka minane mfululizo, aliliambia Nipashe jana kuwa tatizo la watumishi hewa lina sura mbili ambazo zinatakiwa kushughulikiwa na serikali ya awamu ya tano.
Alisema jambo la kwanza ni uzembe na lingine ni mfumo mbovu wa uajiri kwenye sekta ya umma.
“Juhudi hizi zinazofanywa na serikali hivi sasa siyo tiba…serikali ichimbe na ijue chimbuko la watumishi hewa kwa sababu bila kufanya hivyo, baada ya miezi sita wataibuka tena,” alisema.
Alisema ni lazima jitihada za serikali zielekezwe katika kuchimbua kiini na kushughulikia.
“Mimi nafikiri sababu moja inayosababisha watumishi hewa ni uzembe, kwa sababu kama mtumishi akifariki duniua, ofisi inapata taarifa na wanashiriki kwenye maziko, lakini wanasahau kutoa jina lake," alisema Utouh na kuonbgeza:
“Lingine ni mfumo mbovu wa ajira…unapoajiriwa, unaandika taarifa zako zote ambazo zinaonyesha ni lini utastaafu kwa hiyo ilitakiwa kuwapo mfumo ambao kwanza unaweza kutoa ujumbe (wa kustaafu) na ambao utakuondoa kwenye utumishi moja kwa moja, lakini hili halifanyiki.”
Aidha, alisema tatizo lingine la watumishi hewa linatokana na mtandao wa watu kadhaa ambao wananufaika na mishahara hiyo akitolea mfano wa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambaye alikuwa analipwa mshahara zaidi ya mmoja.
Alisema isingewezekana kupata malipo hayo kama idara ya uhasibu pamoja na utawala kutofahamu jambo hilo.
“Hili ni tatizo kubwa na mimi kwa kipindi cha miaka minane nikiwa CAG, nimelipigia kelele kupitia ripoti za ukaguzi…na lipo kila mahali katika ngazi zote, lakini linatofautiana wingi wa watumishi kutokana na wingi wao kwenye idara yao,” alisema.
Kuhusu wanufaika hasa wa mishahara ya watumishi hewa, alisema: “Inawezekana zinagawanywa kwa wahusika wanaojua au zinamfaidisha mtu ambaye ameshaacha au kuachishwa kazi, ambaye hajaondolewa kwenye utumishi wa umma.”
Alisema kutokana na mfumo ulipo sasa, ni vigumu kukosekana kwa watumishi hewa kwa kuwa imekuwa kawaida kwa mtu kufariki dunia na akaendelea kupokea mshahara kwa zaidi ya miaka miwili.
Utouh ametoa angalizo hilo siku chache baada ya serikali kutangaza kubaini wafanyakazi hewa zaidi ya 7,800 katika mikoa mbalimbali ambao wanadaiwa kulipwa zaidi ya Sh. bilioni 7.5.
Mchakato huo ulianza baada ya Rais Magufuli kuwataka wakuu wapya wa mikoa aliowaapisha Machi 15, mwaka huu, kufichua watumishi hewa katika mikoa yao na kuwasilisha taarifa ndani ya siku 15 baada ya kuanza kazi.
Hata hivyo, akitoa taarifa za mkoa wake wa Shinyanga, Kilango alisema haukuwa na watumishi hewa, jambo lililoilazimu Ikulu kufanya uchunguzi zaidi na hadi Jumapili Aprili 10, mwaka huu, ilibaini kuwapo watumishi hewa 45 ambao wamelipwa Sh. milioni 339.9, huku kazi hiyo ikiendelea katika Wilaya ya Ushetu na Shinyanga Vijijini.
Mbali ya Kilango, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Abdul Dachi, naye amesimamishwa kazi kwa kosa la kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu watumishi wa umma hewa mkoani Shinyanga.
Post a Comment