Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemtia hatiani Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) kwa kosa la kumtukana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Kutokana na kumtiwa hatiani Kubenea, mahakama hiyo imempa adhabu ya kukaa nje miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama hilo.
Hata hivyo upande wa Utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala ulisema unakusudia kukata rufaa kutokana na mahakama hiyo kumtia hatiani mteja wao.
Kabla ya kupewa adhabu hiyo, Kubenea aliiomba mahakama hiyo impe adhabu nafuu ambayo itamfanya aendelee kuhudumia wananchi wake.
“Mheshimiwa Hakimu naiomba mahakama yako tukufu inipe adhabu nafuu ambayo itanifanya niendelee kutumikia wananchi wangu na kutimiza majukumu yangu kwa wananchi wangu” alidai Kubenea.
Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Thomas Simba alikubaliana na ombi la mshtakiwa huyo na kumhukumu adhabu ya kukaa nje miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama hilo.
“Kwa kuwa mshtakiwa hii ni mara yake ya kwanza kushtakiwa mahakamani kwa kosa hili, nakubaliana na maombi ya mshtakiwa aliyotoa Mahakamani hapa hivyo anastahili kupewa adhabu ya huruma na mahakama inampa adhabu ya kukaa nje kwa muda wa miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama hili”alisema Hakimu Simba.
Hakimu Simba alisema mbali na adhabu hiyo, Kubenea pia atasaini karatasi ya mahakama ambayo inaonyesha kukubali kwa adhabu hiyo.
“Nafasi ipo wazi kwa upande wa mashtaka kukata rufaa iwapo kama hawajaridhika na adhabu hii” aliongeza hakimu Simba.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu Simba alisema mshtakiwa huyo ametiwa hatiani baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi wa mashahidi watatu kutoka upande wa mashtaka waliotoa mahakamani hapo.
Alisema kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na Shahidi namba moja katika kesi hiyo Paul Makonda, alidai Desemba 14, 2015 katika kiwanda cha TOOKU Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External, alisikika Kubenea akimtolewa lugha chafu kuwa ni kibaka, mjinga, mpumbavu na kwamba nafasi yake ni ya kupewa.
Hata hivyo katika ushahidi uliotolewa na Kubenea, hakimu Simba alisema mshtakiwa alidai kuwa alikwenda katika kiwanda hicho kwa lengo la kutatua mgomo wa wafanyakazi ambao waligoma wakidai nyongeza ya mshahara wao ambao baadhi yao ni wananchi wake.
Hakimu huyo alisema baada ya kuchunguza ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imedhibitisha pasina kuacha shaka kuwa maneno hayo yangeleta uvunjifu wa Amani, na hivyo mahakama ilimtia hatiani kwa lugha ya matusi.
Hata hivyo upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali ,Mtalemwa Kishenyi ulidai mahakamani hapo kuwa hauna kumbukumbu za nyuma kuhusiana na hatia za mshtakiwa.
“Tunaomba mahakama hii itoe adhabu stahiki kwa mujibu wa kifungu cha 89 (i) (a) cha kanuni ya adhabu, sura ya 16” alisema Kishenyi.
Kutokana na maelezo hayo, hakimu Simba alitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwa nini asipewe adhabu.
Hali ilikuwa hivi wakati wa kujitetea Kubenea:
“Mheshimiwa mimi nilienda pale kiwandani katika kiwanda cha TOOKU Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External, kwa nia njema tu ya kutatua mgogoro wa wafanyakazi ambao baadhi yao walikuwa ni wapiga kura wangu wa jimbo la Ubungo”alijitetea Kubenea.
Pia , Mshtakiwa huyo alijitetea kuwa hakukuwa na fujo zilizojitokeza na pia hakuna na nia mbaya wala miadi na aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda hivyo anaiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu.
Vile vile alijitetea kuwa bado wananchi wake wanahitaji awahudumie kwa kuwa ni mbunge wa Ubungo na pia upande wa Jamhuri umekiri kuwa hana rekodi ya mashtaka hivyo aliimba mahakama hiyo impunguzie adhabu.
Kutokana na maombi hayo , hakimu Simba alifafanua kuwa kesi kama hiyo hukumu yake inaweza kuwa ni faini au kwenda jela, au kwenda jela bila faini au mahakama inaweza kumuachia bila masharti yoyoye au kwa masharti maalumu.
“Nimefikira kosa lilivyotendeka na mazingira yake hivyo nakubaliana na mshtakiwa kwamba anastahili kupunguziwa adhabu hii, hivyo atatumikia adhabu ya kukaa nje miezi mitatu kwa masharti ya bila kujihusisha na kosa kama hili” alifafanua Hakimu Simba.
Katika kesi ya msingi, Kubenea anadaiwa kuwa Desemba 14, 2015 katika kiwanda cha TOOKU Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External, alimtolea lugha chafu Makonda kuwa ni kibaka, mjinga, mpumbavu na kwamba nafasi yake ni ya kupewa.
Hali ilivyokuwa mahakamani:
Kubenea alifika mahakamani hapo asubuhi ya saa mbili huku akiambatana na wakili wake, Peter Kibatala na wafausi wake.
Kubenea alikuwa amevalia suti rangi ya kijivu pamoja na viatu vyeusi na miwani.
Hukumu hiyo imechukua muda wa dakika zipatazo 50 ambapo ilianza saa 6:57 mchana na kukamilika saa 7:47 mchana.
Nje ya mahakama:
Kubenea alisema amepokea hukumu hiyo kwa moyo mkunjufu ila wanatarajia kukata rufaa kwa hati ya dharura kupinga mahakama kumkuta na hatia.
Alisema kesi hiyo inafananishwa na kesi ya kisiasa na kwamba yeye ataendelea kusonga mbele katika kuwatumikia wananchi wake ambao walimchangua kwa kura zaidi ya asilimia 87.
“Mimi nimepewa adhabu ya kukaa nje miezi mitatu bila kufanya kosa kama hili na sio kifungo kwa hiyo imeipokea vizuri”alidai Kubenea.
Post a Comment