Loading...

BREAKING NEWS: KILICHOKUWA KIKIPIGANIWA NA KAMBI YA UPINZANI KUPITIA MSEMAJI WAKE GODBLESS LEMA HADI BUNGE LILIPOFANYA MAAMUZI YA KUSTAJABISHA SASA CHA WEKWA HADHARANI NI AIBU TUPU...


AKATA la utata wa mkataba wa utekelezaji wa mradi kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited, limeendelea kutikisa nchi, baada ya jana shughuli za Bunge mjini hapa kusimama kutokana na kuzuiwa kuwasilishwa kwa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyokuwa imesheheni taarifa kuhusu mkataba huo.
Kampuni hiyo ilikuwa inatekeleza mradi wa usimikaji wa vifaa vya mfumo wa utambuzi wa alama za vidole (Automated Fingerprint Identification System - AFIS).
Baada ya kumalizika kwa Kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni jana asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan 'Zungu', alimwagiza Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, kukutana na Kamati ya Kanuni ili hotuba yake aliyopanga kuiwasilisha bungeni ikidhi matakwa ya Kanuni za Bunge.
Hotuba hiyo inahusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Bila kutaja makosa ya kikanuni yaliyomo ndani ya hotuba ya Lema, Zungu pia alimtaka Kiongozi wa Kambi Rasmi Bungeni, Freeman Mbowe, kuungana na Lema kwenda kushauriana na Kamati ya Kanuni ili kutafuta mwafaka wa maudhui yaliyomo katika hotuba hiyo ya upinzani.
"Naomba Kamati ya Kanuni, Mheshimiwa Lema pamoja na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, kukutana na kujiridhisha kuwa maudhui yaliyomo katika hotuba ya Msemaji wa Upinzani, yanakidhi masharti ya uendeshaji wa Bunge hili," alisema Zungu.
Hata hivyo, agizo hilo lilizua mjadala na minong'ono ndani ya Ukumbi wa Bunge, huku baadhi ya wabunge wakisikika wakisema "Lugumi, Lugumi, Lugumi".
Wakati minong'ono hiyo ikiendelea, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisimama na kuomba mwongozo akieleza kuwa hotuba ya Lema ni msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Alisema kumuita katika kamati hiyo pekee haikuwa sawa kwani kilichoandikwa katika hotuba hiyo kilikuwa sawa na kwamba kambi hiyo haipaswi kuelekezwa cha kusema.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, naheshimu maagizo uliyoyatoa kama Mwenyekiti, lakini nasimama hapa kwa niaba ya kambi (ya Upinzani), hii si hotuba ya Mheshimiwa Lema, ni hotuba ya kambi," alisema Mchungaji Msigwa na kuongeza:
"Na kwa mara ya kwanza katika Bunge tunaona kwamba kambi sasa inataka kuambiwa nini cha kuwasilisha mezani.
Na kanuni hazisemi hivyo, sisi tunaandaa kama kambi na kile tunachoona kinafaa kuishauri serikali, ndiyo tunakileta mezani. Tunataka tupate ufafanuzi haya yanatoka wapi, kwamba kamati ikae ianze ku'filter' na kama kuna udhaifu kwenye hotuba yetu, basi huo ni udhaifu wa Kambi ya Upinzani na serikali wanatakiwa watu'challenge'(watupinge) wakati wakitoa majibu."
Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala (CCM), alisema: "Mheshimiwa Msigwa, nafikiri wewe unajua Kiswahili vizuri sana.
Nimesema Kamati ya Kanuni na Lema na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani wakutane, sijasema Kamati ya Kanuni ikaandae hotuba ya upinzani. Nawaomba Mheshimiwa Lema, mpaka sasa hivi nilitegemea mmeshaondoka pamoja na kamati. Naomba muende," alisisitiza Zungu.
Baada ya Lema kuondoka ndani ya Ukumbi wa Bunge, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, aliwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17, iliyofuatwa na taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu wizara hiyo.
Baada ya mwenyekiti wa kamati hiyo, Balozi Adadi Rajabu, kuwasilisha taarifa hiyo, Lema alikuwa hajamalizana na wajumbe wa Kamati ya Kanuni, hivyo hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kushindwa kuwasilishwa.
Kutokana na changamoto hiyo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alisimama na kuomba kikao cha Bunge kiahirishwe.
"Kwa kuzingatia taarifa ambayo umeitoa sasa hivi ndani ya Bunge lako Tukufu, naomba nitumie Kanuni ya 28(2) na (3), kutoa hoja na kuliomba Bunge lako lisitishwe mpaka saa 10 jioni na kutoa muda kwa Kamati ya Kanuni kuweza kuhitimisha shughuli ambayo umeipeleka mbele ya kamati hiyo na baada ya hapo, Bunge hili liweze kuendelea na shughuli kwa kadiri utakavyotoa maelekezo," alisema Jenista.
Baada ya hoja hiyo, Zungu aliwahoji wabunge na kuahirisha shughuli za Bunge hadi saa 10:00 jioni.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa Bunge alitangaza kuwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliombwa kukutana kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mara baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho saa 5:46 asubuhi.
KIKAO KILIPOENDELEA JIONI
Akitoa mwongozo wa kilichotokea asubuhi, Zungu alisema Kamati ya Kanuni ilikutana kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa kujiridhisha kama taarifa ya Lema haikuwa imekiuka Kanuni za Kudumu za Bunge.
Aliwataja wajumbe waliohudhuria kikao cha kamati hiyo kuwa ni Dk. Tulia Ackson (Mwenyekiti) na wajumbe; Freeman Mbowe, George Masaju (pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Andrew Chenge, Jasson Rweikiza, Magdalena Sakaya, Salome Makamba, Zainab Katimba, Balozi Rajabu, Dk. Charles Tizeba, Kange Lugola na Lema (mwalikwa).
"Kamati imepitia na kujadiliana kwa kina kuhusu maudhui ya taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na kubaini imekiuka masharti ya Kanuni za Bunge," alisema Zungu.
Alisema kamati hiyo imeagiza maneno yote yaliyokuwa kwenye taarifa ya Lema kuhusu mauaji ya viongozi wa kisiasa (ukurasa wa 7-9) yaondolewe.
"Mbili, maeneo yote yanayohusu mkataba tata kati ya Kampuni ya Lugumi na Jeshi ya Polisi, yaondolewe. Kamati imependekeza maneno yote yanayoanzia ukurasa wa 10 hadi wa 14 yaondolewe," alisema.
Mwenyekiti huyo wa Bunge alisema kamati imependekeza ukurasa wa 15, aya ya kwanza hadi ya tatu, maneno ya kumhusisha Rais kuhusu kuuzwa kwa nyumba za serikali yaondolewe na litumike neno serikali.
Jambo la nne lililohusu rushwa na Bunge kutumika kulinda wahalifu nchini, Zungu alisema Kamati imependekeza maudhui ya kipengele hicho yanayoanzia ukurasa wa 15 hadi wa 17 yaondolewe kwa kuwa yanakiuka masharti ya Kanuni za Bunge.
"Tano, eneo lingine linahusu kipaumbele kinachohusu tabia za Rais Magufuli na usalama wa nchi. Katika eneo hili, kamati inapendekeza maneno yote yaliyomo kwenye kipengele hiki yanayoanzia ukurasa wa 19 hadi 20 yaondolewe," alisema.
Baada ya kupitia ushauri na mapendekezo ya Kamati kuhusu suala hilo, Zungu alisema kuwa kwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 64(1)(c)(d)(e)(f) ambayo pamoja na mengine, alisema imekata kuzungumzia jambo lololote linalosubiri uamuzi wa mahakama, kutotumia jina la Rais kwa dhihaka, kutozungumzia mwenendo wa Rais na kutosema vibaya au kutoa lugha ya matusi dhidi ya mbunge au mtu mwingine yeyote.
"Baada ya kupitia kutafakari na kwa kuzingatia uamuzi mbalimbali wa Spika kuhusu uzingatiaji wa Kanuni ya 64, na kwa kuwa taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni yaliyobainishwa na Kamati ya Kanuni, yanapingana na kanuni hiyo, namwelekeza Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni aondoe maneno yote yaliyoanishwa hapo juu.
Waheshimiwa wabunge, huo ndiyo mwongozo wangu. Ahsante," alisema.
Baada ya kutolewa kwa mwongozo huo, Lema alipewa fursa ya kuwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, lakini hakuwasilisha chochote zaidi ya kumshukuru mke wake kwa kumtembelea bungeni.
"Kwa sababu ya mwongozo wako huo, maana yake ni kwamba hotuba yangu yote nitakuwa nimeiondoa, basi tu mimi nishukuru kwa mke wangu kufika bungeni, tuendelee na kazi nyingine za Bunge," alisema Lema.
Hata hivyo, baadaye Lema alipewa nafasi ya kuchangia hotuba ya makadirio ya wizara hiyo, na yeye alitumia fursa hiyo kuanza kuzungumzia yale yote aliyotakiwa kuyaondoa, jambo ambalo lilimfanya Zungu kusimama na kumtaka azingatie maelezo aliyopewa awali.
BAJETI YA WIZARA
Awali, akisoma hotuba yake, Kitwanga aliomba kuidhinishiwa Sh. bilioni 864.106 kwa ajili ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha, ambazo pamoja na mambo mengine, zitasaidia idara mbalimbali zilizopo chini ya wizara hiyo ikiwamo kukamilisha mchakato wa Vitambulisho vya Taifa.
Kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 316.126 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo, Sh. bilioni 500.056 za mishahara, wakati Sh. bilioni 47.923 ni kwa maendeleo.
Bajeti ya wizara hiyo imepunguzwa kwa Sh. bilioni 8.597 ikilinganishwa na ya mwaka huu ulio ukingoni ambayo ilikuwa Sh. bilioni 872.703.
Kati ya fedha hizo za bajeti ya mwaka huu, Sh. bilioni 685.86 ndizo zilikuwa zimetolewa na serikali hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, sawa na asilimia 78.59 ya bajeti iliyoidhinishwa.
KITWANGA SIHUSIKI NA LUGUMI
Katika hatua nyingine, Waziri Kitwanga amesema hahusiki na mkataba uliongiwa baina ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi ya kufunga mitambo ya kuchukulia alama za vidole katika vituo vya polisi nchini.
Waziri Kitwanga aliyasema hayo mjini Dodoma jana muda mfupi baada ya kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/17.
Aliitaka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupeleka ushahidi wowote unaomhusisha kuhusika na mkataba huo, naye atafafanua.
“Watu hawajui sheria, mimi sina kigugumizi chochote kuhusu Lugumi, na wala sifanyi kazi kwa magazeti, taarifa ya mkataba huo niliiwasilisha mimi mwenyewe kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali,” alisema Kitwanga.
Alisema hahusiki na mkataba huo na kwamba ni taarifa za watu wenye nia mbaya naye wanaotaka kumchafua.
Hata hivyo, awali Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu, akitoa taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/17, alisema Kamati ya Mambo ya Nje inatambua uzito na umuhimu wa suala hilo.
Alisema kwa kuwa suala hiyo liliibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na kifungu cha 14(a) na kifungu cha 16 cha nyongeza ya nne ya Kanuni za Kudumu za Bunge kimeipa jukumu PAC kushughulikia matatizo sugu ya matumizi mabaya ya serikali, hivyo ni vyema PAC ikaachwa ikaendelea kushughulikia suala hilo.
“Kwa kuwa suala hili tayari linashughulikiwa na Kamati ya PAC, hivyo basi ni vyema Kamati ya Hesabau za Serikali ikaachwa ikaendelea kushughulikia hoja ya CAG kwa utaratibu wa uendeshaji shughuli zake,” alisema Balozi Adadi.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, alisema kuwa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jana ilitaka kuwasilisha hotuba bungeni ambayo ilikuwa inamwomba Rais John Magufuli kumrejesha nchini aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mathias Chikawe, ambaye kwa sasa ni Balozi nchini Japan, kuwa alihusika katika utiwaji sahihi wa mkataba huo baina ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi.
Alisema Kambi ya Upinzani inamtaka Rais Magufuli kuchukua hatua za kisheria dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Said Mwema, mmiliki wa Kampuni ya Lugumi na viongozi waandamizi katika serikali ya awamu ya nne waliotajwa kuhusika katika mkataba huo.
Aprili 5, mwaka huu, PAC ilikutana na viongozi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kupitia mahesabu yao na kubaini kuwapo kwa mkataba huo tata ulioingiwa baina ya jeshi hilo na Kampuni ya Lugumi wa ufungaji wa mashine za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo vya polisi 108 wenye thamani ya Sh. bilioni 37.
Lakini, inadaiwa ni vituo 14 ndivyo vilivyofungwa mashine hizo wakati kampuni hiyo ililipwa Sh. bilioni 34 sawa na asilimia 99 ya fedha zote, hali iliyoilazimu PAC kuhitaji maelezo ya mkataba huo.
Hata hivyo, Aprili 11, mwaka huu Jeshi la Polisi halikuwasilisha mkataba huo kama ilivyoagizwa, hali iliyowalazimisha wajumbe wa PAC kuliandikia barua na kulipa siku tatu hadi Aprili 15 , mwaka huu liwe limewasilisha mkataba huo.
Ilipofika Aprili 15, mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliingilia suala hilo na kueleza kuwa mkataba huo utawasilishwa bungeni Dodoma.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilishindwa kuwasilisha mkataba huo, badala yake liliwasilisha maelezo ya mkataba, hali iliyoilazimu Kamati ya PAC kuunda kamati ndogo ya watu tisa itakayochunguza kwa kina suala hilo na kutakiwa kufanya kazi kwa siku 30.
Wajumbe tisa wa kamati hiyo ndogo ni; Japhet Hasunga (Vwawa-CCM), wengine wa CCM ni Livingstone Lusinde (Mtera), Stanslaus Mabula (Nyamagana), Haji Mponda (Malinyi) na Hafidh Ali Tahir (Dimani).
Wabunge wa upinzani waliopo katika kamati hiyo ni Naghenjwa Kaboyoka (Same Mashariki-Chadema), Musa Mbaruk (Tanga Mjini-CUF), Tuza Malapo (Viti Maalum-Chadema) na Khadija Nassor Ali (Viti Maalum-CUF).

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright NEWZ | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top