Dar es Salaam. Wakati hali ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ikielezwa ni mbaya na haina mkakati wa kujinusuru, baadhi ya mawaziri waliowahi kuongoza wizara inayolisimamia wametupiana mpira kuhusu nani anawajibika kwa hilo.
Mawaziri hao jana kwa nyakati tofauti walitoa madai hayo siku moja baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubainisha ufisadi ukiwamo hatua ya ndege moja iliyokodishwa Oktoba 2007 kugharimu zaidi ya Sh90 bilioni na kufanya kazi kwa miezi sita tu.
Ripoti hiyo iliyotolewa juzi na CAG, Profesa Mussa Juma Assad inaeleza kuwa hadi sasa ATCL haina mkakati wowote wa kina wa kujifufua na kwa zaidi ya miaka tisa imekuwa ikipata hasara.
Kauli ya Chenge
Aliyekuwa Waziri wa Miundombinu mwaka 2008, Andrew Chenge alipoulizwa alijibu kwa kifupi: “Kama taasisi ipo, haipendezi kusema haipo hivyo itafutwe ofisi ya waziri yenye dhamana ya suala hilo kwa sasa. Yale yaliyofanyika kipindi hicho yalifanyika wakati Serikali ipo, ofisi ya waziri ilikuwapo, sasa niwafundishe kitu, kawaulizeni hao mimi siwezi ku comment (kusema).”
Omar Nundu
Wakati Chenge aliyejiuzulu wadhifa huo wakati wa sakata la rada akisema hayo, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi katika kipindi cha Novemba 2010 hadi Mei 2012, Omar Nundu alisema alijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kulifufua shirika bila mafanikio.
“Nilipokuja hapa nilikuta ndege zote zimelala, ilikuwapo ndege moja mbovu nyingine inatengenezwa Afrika Kusini, nikaamua kujitolea kulifufua shirika hilo,” alisema.
Alisema alipoteuliwa kuongoza wizara hiyo aliikuta katika hali mbaya kuanzia bandari, reli na usafiri wa anga.
“Nilitaka Air Tanzania ifanye kazi, nauli ipungue shirika lijiendeshe, hata lisipofufuka lakini nilitaka usafiri uchanganye,” alisema.
Kadhalika, Nundu alisema alifanya mambo mengi kwenye wizara hiyo ikiwamo kumuondoa Mhindi aliyeshika reli, jambo ambalo anadai alifanikiwa na hatimaye kufufua usafiri wa reli. Ingawa hakumtaja lakini wakati akiwa waziri, Serikali ilivunja mkataba na kampuni ya Rites ya India iliyokuwa ikiendesha Shirika la Reli Tanzania – TRL.
Kuhusu ATCL, alisema aliamua kuibadili kwa kumweka mkurugenzi makini: “Nilipaona pachafu nikatafuta mtu safi lakini nilipotoka na yule akaondolewa (Paul Chizi) kwa tuhuma lukuki.”
Alipoulizwa anashauri nini alisema: “Hata nikitoa ushauri nitasaidia nini wakati mliniona sifai, sasa niwashauri nini, leo nitashauri nini. Mimi nilijitolea kusimamia na wala si kutoa ushauri.”
Samuel Sitta
Aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, kuanzia Januari 2015 hadi Novemba 2015, Samuel Sitta alisema hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa aliishika wizara hiyo kwa muda mfupi.
“Niliishika hiyo wizara kwa mfupi sana wakati wa uchaguzi. Wapo waliowahi kuishika kwa muda mrefu, ukiniuliza mimi utakuwa unanionea,” alisema Sitta.
Alisema wapo mawaziri wanaofahamu mikataba hiyo zaidi yake na kuwa yeye haifahamu kwa undani.
“Kama unautaka ukweli, wewe muulize Nundu au (Dk Harrison) Mwakyembe aliyeko serikalini sasa hivi. Hao wanajua zaidi kuliko mimi, mimi unanionea tu,” alisema.
Shukuru Kawambwa
Waziri mwingine aliyewahi kuongoza wizara hiyo, Dk Shukuru Kawambwa alisema ripoti ya CAG imeibua mambo yaliyokuwapo wakati alipokuwa waziri.
“Niliyaona nikapunguza nusu ya wafanyakazi, mpango ulikuwa ni kuwaondoa wasio na tija na kuajiri wapya ambao watashindanishwa kwa vigezo,” alisema.
Alisema alianza mazungumzo na mwekezaji kutoka Singapore ambaye aliahidi kuingia ubia na Serikali ili kulifufua shirika hilo.
Alisema mwekezaji huyo ndiye aliyenunua ndege mbili aina ya Bombadier Q ambazo moja inafanya kazi mpaka sasa na nyingine imeharibika.
Hata hivyo, Dk Kawambwa ambaye ni Mbunge wa Bagamoyo (CCM) alisema mwekezaji huyo alitakiwa kusaini mkataba Juni 30, 2009 lakini alikacha dakika za mwisho.
“Ilikuwa ndoto yangu kulifufua shirika, ningestaafu kwa amani nikaja Bagamoyo nikiwa na furaha kuwa nimeibadili ATCL lakini Mungu hakupenda,” alisema.
Profesa Makame Mbarawa
Waziri wa sasa wa Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema hata kabla ya ripoti hiyo, anachotaka ni kuifumua na kuiunda upya ATCL.
Alisema katika muundo huo mpya, kutakuwa na kununua ndege mpya, kubadili wafanyakazi na kuwaondoa wale wasio na tija. “Kwa kifupi tunaanza kila kitu upya, hivyo ndivyo tunavyofanya,” alisema.
Mwakyembe ambaye pia amewahi kuwa waziri katika wizara hiyo hakupokea simu jana.
Kaimu Mkurugenzi ATCL
Kaimu Mkurugenzi wa ATCL, Rogate Mfinanga alisema hawezi kuzungumza lolote kuhusu ripoti hiyo hadi atakapoisoma kwa undani na kujua muktadha wake na hitimisho lililotolewa na CAG.
“Kuna vitu tulishaanza kuvifanyia kazi vingine vimechukua muda mrefu kama shirika kuna mambo mengi na siwezi kuyasema hapa kwa simu,” alisema.
Ndege ilivyotafuna…
Katika ukaguzi wake, CAG amebainisha namna shirika hilo lilivyotafunwa hasa baada ya kuonyesha lilivyoingia mkataba na kampuni ya Wallis Trading Co Limited kukodi ndege aina ya Airbus A320-214 ambao haukufuata taratibu.
Mkataba huo uliitaka kampuni hiyo kuilipa Wallis Dola 370,000 za Marekani kila mwezi kwa ajili ya malipo ya kukodi ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 150.
Wakati mkataba huo ukifanyika, ATCL ilikuwa na miezi michache baada ya Serikali kurudisha asilimia 49 ya hisa zilizokuwa zimeuzwa kwa Shirika la Ndege Afrika Kusini (SAA) kama sehemu ya kutekeleza ubia katika sera za ubinafsishaji.
Profesa Assad alisema vitengo vya ufundi vya ATCL na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCAA) ambavyo hutakiwa kukagua ndege kabla ya mkataba kufikiwa, vilifanya ukaguzi kati ya Januari 14 na 22, 2008 wakati makubaliano ya ukodishaji tayari yameshafanyika.
Hata hivyo, baada ya ukaguzi, TCCA ilibaini kuwa ndege hiyo ilikuwa haijafikisha viwango vinavyotakiwa na ilimpa maelekezo mkodishaji kwenda kuirekebisha kabla ATCL haijaipokea.
Profesa Assad alieleza kuwa menejimenti ya ATCL pia ilipuuza ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alioutoa Oktoba 8, 2007 kabla ya mkataba huo kufikiwa na Wallis.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mkodishaji alikubali kufanyia matengenezo ndege hiyo Februari, 2008 lakini hakuikabidhi kwa ATCL hadi ilipofika Mei mwaka huo baada ya Serikali kutoa barua ya dhamana ya Dola 60 milioni za Marekani (Sh129 bilioni kwa thamani ya sasa ya Dola).
Katika kipindi hicho cha miezi saba hadi Mei, 2018 wakati ndege ikiwa matengenezoni, CAG anasema ATCL iliendelea kulipia kodi ya kila mwezi hivyo kutengeneza limbikizo la deni la Dola 2.59 milioni za Marekani (Sh5.5 bilioni).
“Ndege ilifanya kazi kwa miezi sita hadi Novemba 2008. Ilipofika Desemba 2008, ilipelekwa katika Kampuni ya Ndege Mauritius kwa uchunguzi mkubwa wa kiufundi, ilikaa hadi Juni 2009. Julai 2009, ilihamishiwa kwa Shirika Ndege Ufaransa kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa kitaalamu ujulikanao C+12.”
Hata hivyo, makadirio ya awali ya matengenezo ya ndege hiyo ya Dola 593,560 za Marekani yalipaa baada ya kutengenezwa na kuwa Dola 3 milioni sawa na Sh6.4 bilioni huku mkodishaji akichangia Dola 300,000 za Marekani pekee na kuacha mzigo wote kwa ATCL.
Hata baada ya matengenezo kukamilika, ndege hiyo haikurudishwa Tanzania kutokana na ATCL kushindwa kulipa gharama husika na ilikaa kwa kipindi chote cha mkataba hadi Oktoba 2011 baada ya Serikali kuusitisha.
“Wakati mkataba wa kukodi unasitishwa, gharama kwa muda wa miezi 43, ambayo ndege hiyo ilikuwa chini ya matengenezo zilifikia Dola za Marekani 15.9 milioni (Sh34.2 bilioni).
“Jumla ya gharama, ikijumuishwa na ada ya kila mwezi ya kukodi na gharama nyingine kama vile riba, ilifikia Dola za Marekani 42.45 milioni (91.2 bilioni kwa viwango vya sasa).”
CAG alishawahi kupendekeza hatua kali zichukuliwe kwa wote waliohusika kuiingiza Serikali kwenye biashara ‘isiyozaa matunda’ katika ukaguzi wa mwaka wa fedha wa 2011/2012 na kusababisha deni kukua mwaka hadi mwaka kutoka Dola 39 milioni mwaka 2012 hadi dola 41.46 milioni za Marekani.
Mkaguzi huyo alitaka Serikali kulijadili deni hilo na kampuni ya Wallis ili kuomba kama kuna uwezekano kwa kulifuta kwa vigezo kwamba Tanzania haikunufaika lakini hilo halijatekelezwa. Tayari kuna kesi mahakamani inayohusu sakata hilo la ukodishaji ndege.
Mbali na malimbikizo ya madeni, ATCL ina wafanyakazi 231, kati yao 127 wana mikataba ya kudumu.
Ripoti hiyo ya mwaka wa fedha unaoishia Juni, 2015 inaeleza kuwa ATCL haina vyeti muhimu vya usafiri wa anga na sasa siyo mwanachama wa Shirika la Usafiri wa Anga la Kimataifa (Iata) baada ya kushindwa kufuata taratibu na kanuni za usafiri wa anga (Iosa). Kwa sasa ATCL ni mwanachama wa Iata kwa kupitishia ndege tu.
Profesa Assad anaeleza kuwa ATCL ina hali mbaya ya kifedha kutokana na madeni lukuki huku chanzo chake cha mapato kikiwa ni tiketi na fedha kutoka wizara mama. Hadi Mwaka 2014, ATCL ilikuwa na deni kubwa lililofikia Sh140 bilioni lakini baada ya mazungumzo na wadai wake lilipungua na kufika Sh111 bilioni.
Post a Comment