Amesema, kwa namna Rais Magufuli anavyoendesha nchi, taifa linahitaji maombi ya haraka kuhakikisha anarudishwa kwenye mstari wa maadili kwa manufaa ya nchi.
Akisoma Makadirio na Mapato katika Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Lema ambaye ni msemaji wa kambi ya upinzani kwenye wizara hiyo amesema, Rais Magufuli ataumiza watu wengi.
“Wakati Taifa letu linapita kwenye changamoto nyingi kama vile ukosefu wa sukari, umeme, umasikini, mizigo kupungua bandarini, madini ya Tanzanite kuanguka bei na ubadhirifu uliokithiri katika mfumo wa utawala. Rais mwenyewe ameonekana kufuatilia na kufanyia kazi habari za kwenye mitandao ya kijamii.
“Kwa tabia hii ya Rais Magufuli, kama Taifa tunahitaji maombi haraka, kwani Rais ataumiza watu wengi sana kwa kufuatilia maneno ya mitaani kwa njia mbalimbali , kwani kwa madaraka aliyonayo Rais bila shaka ataumiza watu wengi.
“Mfano, Sakata la Mke wa Waziri Mahiga na Trafiki barabarani. Ni jambo dogo sana na la karaha kuona linazingatiwa na Rais,” amesema Lema.
Amesema, haikuwa busara Rais Magufuli kukemea familia ya waziri wake mbele ya vyombo vya habari na kuagiza askari huyu kupandishwa cheo bila kujua historia ya utumishi wake.
Lema alikumbusha kwamba, wabunge walipoanza vikao vya Kamati za Bunge, vyombo vya habari vilimnukuu Rais Magufuli akielezea mpango wake wa kuanza kurekodi mawaziri wake wanaolalamika juu ya staili yake ya uongozi.
“Kwa hiyo leo ukienda kwenye ofisi za mawaziri unaona, hofu, mashaka, kutokujiamini, mambo yatakayo punguza ufanisi, ubunifu na uhuru katika utendaji wao, jambo linalopeleka Taifa kuzorota katika nyanja zote kwa utumishi wa umma jambo ambalo ni hatari kwa Taifa,” amesema.
Akizungumzia mashaka ya nchi Lema amesema,
Taifa letu liko katika mashaka na kuwa, serikali inaufahamu ukweli huu.
“Taifa hili lina utulivu unaosabishwa na hofu inayojengwa kwa mabavu na silaha na sio amani, kuna mateso makubwa wanayoyapata wananchi wa Taifa hili kila siku, umasikini, njaa, ukandamizwaji, ubaguzi, uonevu, udhalilishwaji na mateso ya jinsi mbali mbali kutokana na kukosa uongozi unaojali maisha ya Watu,” amsema na kuongeza;
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni baada ya uchambuzi na tathimini ya “Hali ya Usalama na Amani ya Nchi yetu” kabla wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015, tumebaini kuwa nadharia na mwenendo wa demokrasia ya vyama vingi hapa nchini iliwekwa kando.
“… na badala yake sura nzima ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015, uligeuka kuwa ‘Military Operation’ yaani ‘Operesheni ya Kijeshi’ kwa kisingizio cha kulinda amani.”
Lema amesema, mnyonge anayelia moyoni kwa huzuni ya kuonewa ni hatari kwa usalama wa nchi na dunia na kwamba, vikundi vingi vya uhalifu duniani kwa asilimia kubwa vimesababishwa na utawala wa kibabe, uonevu na ukandamizwaji usiovumilika na huko ndiko tunakoelekea kama Taifa.
Amesema, “matendo mabaya haya yaliofanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita Zanzibar na Tanzania Bara ni ishara ya watawala kuelekeza Nchi yetu katika mapigano ya sisi kwa sisi katika siku za usoni.
“Unapokuwa na Jamii inayoamini kuwa mfumo wa demokrasia hauwezi kuwapa wananchi viongozi wanaowataka, maana yake ni dhahiri kwamba unaanza kuifundisha jamii hiyo kufikiri njia mbadala ya mabadiliko katika Nchi.”
Amesema kuwa, Tume ya Uchaguzi inayotiliwa shaka na jamii ni hatari kwa usalama wa nchi na kwamba, ni muhimu kwa taifa kutafakari uwepo wa katiba ya wananchi na Tume Huru ya Uchaguzi itakayorudisha imani ya Wananchi katika uchaguzi wa kidemokrasia.
“Mungu adhihakiwi apandacho mtu ndicho avunacho, utulivu mnaouona Zanzibar na kwingine kokote kule kuliko na ukandamizaji ni nafsi zinazojadili mwelekeo mpya wa maisha yao katika utawala wa nchi yao.
“Zanzibar mmeshinda uchaguzi kwa hila na sio kwa haki, wekeni kumbukumbu maneno ya Kambi Rasmi ya Upinzani leo kuwa, ipo siku Zanzibar itakuwa ni sehemu ngumu ya kuishi binadamu kama hamtachukua hatua sasa ya kurekebisha mlichokifanya Zanzibar na Tanzania Bara katika uchaguzi uliopita,” amesema.
Hata hivyo amehoji kwamba, kwa namna mambo yanavyoendeshwa nchini, je kuna matarajio ya taifa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwa njia ya kidemokrasia?
Post a Comment